Na mwandishi wetu, Gazetini
VICHOCHEO vya maendeleo ni nyenzo muhimu katika kuongeza kasi ya kufikia malengo ya Dira 2050. Kwa kutambua hilo, Dira hii imebainisha vichocheo vitano vya maendeleo, ambavyo ni usafirishaji fungamanishi, nishati, sayansi na teknolojia, utafiti na maendeleo mageuzi ya kidigitali.
Je, nini maana ya usafirishaji fungamanishi? Na ni kwa namna gani unaweza kuchagiza kasi ya kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050? Makala haya yanaeleza.
Usafirishaji fungamanishi ni mfumo mzima wa usafirishaji wa bidhaa, utoaji wa huduma, shughuli za watu, na upatikanaji wa taarifa. Ni mfumo unaolenga kuimarisha uratibu na usimamizi wa mtiririko wa bidhaa, huduma, taarifa na rasilimali kupitia mnyororo wa usambazaji unaoanzia kwenye uzalishaji hadi kwa mtumiaji wa mwisho, kwa ufanisi na kwa gharama nafuu.
Aidha, katika kufanikisha ufanisi wake, usafirishaji fungamanishi unahitaji ushirikiano thabiti kati ya usafirishaji, wadau wa uzalishaji, uhifadhi, usambazaji, na watoaji wa huduma.
Wakati Tanzania ikidhamiria kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi, kuimarisha mfumo wa usafirishaji ni hatua muhimu kwa maendeleo endelevu.
HATUA ZILIZOPIGWA
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya usafirishaji kwa kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati, kufanya mageuzi ya kimuundo na kuimarisha matumizi ya teknolojia.
Hatua hizo ni pamoja na uwekezaji katika mtandao wa Barabara, reli ya kisasa ya SGR na upanuzi wa bandari na viwanja vya ndege.
Ni katika hilo, Serikali imeweza kuboresha utendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania, ikiwamo ununuzi wa ndege za kisasa na kuongeza safari za ndani na nje.
Kwa namna moja au nyingine, uwekezaji huo umeimarisha miundombinu ya usafirishaji ndani na nje ya nchi, pia kuiunganisha Tanzania na nchi jirani, kukuza biashara za kikanda na ushirikiano wa kiuchumi.
Wakati huo huo, kuanzishwa kwa vituo vya huduma za pamoja mipakani kumeimarisha biashara, huku matumizi ya teknolojia za kidigitali yakiboresha usimamizi wa kodi na vibali, udhibiti wa hesabu, ufuatiliaji wa mizigo, na ufanisi katika mfumo wote wa usambazaji.
CHANGAMOTO
Hata hivyo, gharama za usafirishaji pekee ni kati asilimia 35 hadi 45 ya gharama zote za kuagiza bidhaa kutoka nje. Hii inaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye gharama kubwa zaidi za uingizaji wa mizigo duniani.
Pia, bado kuna kiwango kikubwa cha ucheleweshaji wa kupakua na kusafirisha mizigo kutokana na uhaba wa vifaa, maghala na mtandao wa usafirishaji usio imara.
Sambamba na hayo, mfumo wa sheria na taratibu za usafirishaji nao una changamoto kadhaa, zikiwamo udhibiti wa kukithiri na utitiri wa kodi na sheria nyingine ndogondogo za serikali za mitaa zinazokinzana na sheria kuu za Serikali.
Kutatua changamoto hizi ni muhimu katika kuboresha sekta ya usafirishaji, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuifanya Tanzania kuwa na ushindani mkubwa zaidi katika biashara za kikanda na kimataifa.
MATARAJIO
Mosi, kufikia mwaka 2050, matarajio ni Tanzania kuwa lango kuu la biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika, ikitumia nafasi yake ya kijiografia kuhakikisha ufanisi wa biashara za mipakani na kuimarisha ushirikiano.
Pili, ni kuiona Tanzania ikiongoza kwa biashara ya usafirishaji, ikiunganisha nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini na masoko ya kimataifa.
Tatu, Tanzania kuwa mtandao wa usafirishaji fungamanishi wenye mfumo wa kisasa na shindani, unaounganisha shoroba za kiuchumi ili kuwezesha biashara za ndani na za kimataifa kwa ufanisi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika sekta ya usafirishaji.
Nne, nchi inayotoa huduma za viwango vya kimataifa, shindani na ikitumia teknolojia za kisasa za kidigitali ili kuongeza ufanisi na kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa katika mnyororo wa thamani.
Tano, Tanzania yenye mazingira bora ya usimamizi wa usafirishaji yanayorahisisha taratibu za forodha, kupunguza urasimu na vikwazo, kuzingatia viwango vya kimataifa, na kuendana na kasi ya maendeleo katika sekta ya usafirishaji.
Sita, Tanzania kuwa na mtandao jumuhishi wa usafirishaji wenye miundombinu inayozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu ili kutoa fursa sawa kwa wote katika biashara za ndani na za kimataifa.


