16.7 C
New York

Sura za makocha wapya kunogesha AFCON 2027

Published:

CAIRO, Misri

UKIACHA Tanzania, Kenya na Uganda ambazo ni wenyeji, timu zingine 21 zinasaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Mataifa ya Afrika [AFCON 2027].

Kwa upande mwingine, yamefanyika mabadiliko makubwa katika mabenchi ya ufundi ya nyingi za taifa kuelekea fainali hizo za Shirikisho la Soka Afrika [CAF].

Herve Renard [57], kocha pekee kuwahi kutwaa ubingwa wa AFCON akiwa na timu mbili tofauti, amerejea kwenye benchi la Ivory Coast ikiwa ni miaka 11 imepita tangu alipoipa ubingwa.

Senegal, kwa upande wao, wamempa ajira kocha Patrick Vieira. Ni kiungo wa zamani wa timu ya Taifa ya Ufaransa na alikuwa kikosini wakati wanatwaa Kombe la Dunia mwaka 1998. Vieira [50], ni kama amerudi nyumbani kwani alizaliwa Senegal.

Claude Le Roy [78], kocha aliyeipa Cameroon ubingwa wa AFCON mwaka 1988, amerejea kwenye benchi la Congo-Brazzaville. Ni miaka mitano imepita tangu alipoondoka kwenye timu hiyo na hivi karibuni alikuwa akiinoa Togo.

Cape Verde iliyofanya makubwa kwenye fainali za Kombe la Dunia baada ya kufika hatua ya 32 Bora, haipo tena na kocha wake wa muda mrefu, Bubista. Aliyekuwa msaidizi wake, Humberto Bettencourt, ndiye anayeiongoza.

Tunisia nayo ina kocha mpya, Moin Chaaban, ambaye aliwahi kupata mafanikio makubwa akiwa na klabu za Esperance [Tunisia] na Berkane [Morocco].

Chaaban amechukua nafasi ya Sabri Lamouchi ambaye alifukuzwa baada ya mechi moja tu wakati wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu na Renard akaajiriwa kwa muda.

Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ imempa kazi kocha mkongwe, Pitso Mosimane, ambaye aliwahi kuinoa miaka 14 iliyopita. Alifuzuzwa baada ya kikosi hicho kushindwa kufuzu fainali za AFCON 2012.

Algeria nayo ina sura mpya kwenye benchi la ufundi. Aliyepewa majukumu kwa sasa ni Brahim Hemdani ambaye amechukua nafasi ya kocha Vladmir Petkovic.

Burkina Faso imemchukua aliyekuwa kocha wa Morocco, Amir Abdou, wakati Angola imekabidhi benchi lake la ufundi kwa kocha aliyepa Senegal ubingwa wa AFCON 2021, Aliou Cisse, ambaye hivi karibuni alikuwa akiinoa Libya.

Ukiacha upande huo, fainali zijazo za AFCON 2027 zitawakosa baadhi ya mastaa kwani waliamua kustaafu kuzitumikia timu zao za taifa baada tu ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.

Mfano; Riyad Mahrez hatoonekana kwenye kikosi cha Algeria, kama ambavyo Senegal haitokuwa na kipa Edouard Mendy ambaye naye alitangaza kustaafu timu ya taifa baada ya Kombe la Dunia mwaka huu.

Ni kama ambavyo Tunisia imeyaanza maisha mapya bila huduma ya staa wake, Ellyes Skhiri. Taifa hilo linasaka tiketi ya kushiriki AFCON kwa mara ya 18 mfululizo.

Gabon nayo itaikosa huduma ya straika wake, Pierre-Emerick Aubameyang. Nyota huyo wa zamani wa Arsenal amestaafu kuitumikia timu ya taifa kwa madai kuwa hapewi heshima anayostahili.

Related articles

Recent articles