26 C
New York

Rais Samia azindua tume ya uchunguzi wa ghasia za uchaguzi 2025

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amezindua Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukaji wa Sheria katika matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akiitaka kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na bila kuingiliwa ili kubaini ukweli kuhusu matukio hayo.

Tume hiyo yenye wajumbe sita imezinduliwa leo Ijumaa, Agosti 7, 2026, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Kabla na Baada ya Uchaguzi Mkuu.

Uzinduzi huo umefanyika siku 106 baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya Tume ya Jaji Chande Aprili 23, 2026, na siku 262 tangu kutangazwa kwa mchakato wa kuundwa kwa tume hiyo mnamo Novemba 18, 2025.

Hii ni tume ya pili kuundwa kuchunguza matukio yaliyotokea katika kipindi cha uchaguzi wa Oktoba 29, 2025. Hatua hiyo imekuwa ikikosolewa na baadhi ya asasi za kutetea haki za binadamu pamoja na vyama vya upinzani, ikiwemo Chadema.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia alisema ana imani wajumbe walioteuliwa watatumia taaluma, uzoefu na viapo vyao vya kazi kutekeleza jukumu walilopewa kwa haki na ufanisi.

“Ni imani yangu kwamba majaji hawa watatumia taaluma, uzoefu na viapo vyao kutekeleza kazi hii kwa weledi, umakini na uadilifu mkubwa. Endapo kutakuwa na ulazima wa kuongeza muda, tutalifanyia kazi jambo hilo,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia aliwataka Watanzania kutoa ushirikiano unaohitajika kwa tume hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na ufanisi.

“Katika hili niwasihi sana Watanzania wote kutoa ushirikiano unaohitajika na tume katika kutekeleza majukumu yao. Tuisaidie tume hii iweze kufanya kazi zake na tusiisumbue,” amesema.

Tume hiyo imepewa siku 150 kukamilisha uchunguzi wake na kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu yake, ikitarajiwa kubaini wahusika wa ghasia na ukiukaji wa sheria uliotokea wakati na baada ya uchaguzi huo.

Tume hiyo inaongozwa na Jaji Mstaafu Shaban Ali Lila kama Mwenyekiti. Wajumbe wengine ni Jaji Petrus Tilainge Damas kutoka Namibia, Jaji Barishaki Cheborion kutoka Uganda, pamoja na Majaji Wastaafu Godemas, Awadh Mohammed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari kutoka Tanzania.

Related articles

Recent articles