21 C
New York

Wagombea sita, nani Katibu Mkuu UN?

Published:

NEW YORK, Marekani

BAADA ya miaka 10 ya kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, atakabidhi kijiti hicho kwa mtu mwingine ifikapo Desemba 31, 2026.

Kwa sasa, kuna wagombea sita wanaosaka ushawishi wa kura ili kupokea kijiti cha Guterres, kila mmoja akifahamu kuwa Katibu Mkuu wa UN ni nafasi nyeti ndani ya Taasisi hiyo. “Katibu Mkuu ni mwanadiplomasia, mwanaharakati, mtumishi wa umma, na Mtendaji Mkuu,” kwa mujibu wa UN.

UN inaelekea katika mabadiliko ya nafasi ya Katibu Mkuu huku Umoja huo ukiwa na miaka 80 tangu kuanzishwa kwake. Je, nani kukalia kiti cha Guterres?

MICHELE BACHELET

Mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya urais katika Taifa la Chile. Bi. Michele alishika wadhifa huo 2006-2010 na 2014-2018. Anasaka rekodi nyingine ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Katibu Mkuu wa UN. Katika Uchaguzi wa UN mwaka 2016, Guterres aliwapiku wanawake kadhaa waliowania naye.

“Kama nitakuwa mkweli, dunia haikuwa tayari (mwanamke kuwa Katibu Mkuu wa UN mwaka 2016). Naamini kwa sasa mambo yamebadilika,” amesema mwenye umri wa miaka 74, ambaye aliwahi kuwa Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN kuanzia mwaka 2018 hadi 2022.

RAFAEL MARIANO GROSSI

Mwanadiplomasia wa kimataifa wa Argentina, ambaye kwa miaka mingi amekuwa kwenye sekta ya nishati ya nyuklia na atomi ndani ya UN.

Masuala ya nyuklia yanashika kasi duniani, na wakati mwingine kuzalisha migogoro kama huu wa Marekani na Iran, hivyo Grossi anajitaja kuwa ni mtu sahihi kuiongoza UN.

“Hii inanipa faida zaidi. Unapaswa kuielewa dunia unayoishi,” alisema Grossi katika moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari.

MARIA FERNANDA ESPINOSA

Mzaliwa wa Hispania mwenye uraia wa Ecuador. Akiwa na umri wa miaka 61, anaamini anatosha kuvaa viatu vya Guterres.

Maria aliyewahi kuwa Rais wa Mkutano Mkuu wa UN, anasema Taasisi hiyo inahitaji mabadiliko makubwa, kinyume chake inaweza kufa.

Changamoto kubwa inayoiona ni taasisi hiyo kukosa fedha. “Ni aidha mabadiliko au kifo,” alisema Maria akihojiwa na waandishi wa habari.

REBECA GRYNSPAN

Alikuwa Makamu wa Rais wa Costa Rica kuanzia mwaka 1994 hadi 1998 na sasa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Biashara na Maendeleo wa UN (UNCTAD).

UNCTAD ni kwa ajili ya kutetea ushirikishwaji na masilahi ya nchi zinazoendelea katika biashara za kimataifa.

Moja ya mambo yaliyompa sifa ni katazo lake kwa nchi wanachana kununua nafaka zinazotoka Ukraine wakati huu nchi hiyo ikiwa kwenye vita na Urusi. Kwamba mali hizo zimekuwa zikiibiwa na maadui na Ukraine.

MACKY SALL

Alikuwa Rais wa Senegal kuanzia mwaka 2012 hadi 2024, ikikumbukwa pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo kabla ya kuingia Ikulu.

Sall alipata pigo kubwa katika muhula wake wa pili wa urais mwaka 2021 baada ya maandamano makubwa ya raia kupinga hatua ya Serikali yake kumfunga jela mwanasiasa wa upinzani, Ousmane Sonko.

Sall atakumbukwa pia kwa jaribio lake la kusogeza mbele Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2024, hivyo kusababisha maandamano makubwa.

CAROLYN RODRIGUES BIRKETT

Alitamgaza nia yake Juni, 2026. Bi. Carolyn ni mjumbe wa kudumu wa nchi ya Guyana ndani ya Umoja huo wa Mataifa.

Vilevile, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali nchini Guyana, ikiwamo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi hiyo inayopatikana katika Bara la Amerika.

Hivi karibuni, Rais wa Guyana, Irfaan Ali, aliweka wazi kuwa wanamuunga mkono bi. Carolyn katika safari yake ya kuwania nafasi ya kuwa Katibu Mkuu wa UN.

Related articles

Recent articles