19.4 C
New York

Tanzania yashiriki mkutano wa AU kujadili ufadhili wa maendeleo ya viwanda

Published:

Na Ramadhan Hassan, Gazetini

NAIBU Waziri wa Fedha, Mshamu Ali Munde, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri wa Umoja wa Afrika (STC) unaojadili masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini unaofanyika Abidjan, Côte d’Ivoire.

Mkutano huo wa Julai 23 hadi 24, 2026, unawakutanisha mawaziri wa fedha, biashara, viwanda, madini, magavana wa benki kuu na viongozi wa taasisi za Umoja wa Afrika kujadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya viwanda kupitia upatikanaji wa rasilimali fedha, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.

Masuala yatakayojadiliwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa fedha za maendeleo ya viwanda, usimamizi wa deni la umma, ukusanyaji wa mapato, kuimarisha masoko ya mitaji, ushiriki wa sekta binafsi pamoja na mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa ili nchi za Afrika zipate rasilimali kwa masharti nafuu.

Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ali Munde.

Mkutano huo pia utajadili athari za migogoro ya kimataifa kwa uchumi wa Afrika, maendeleo ya viwanda, ujenzi wa shoroba za kimkakati na utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Ushiriki wa Tanzania unatoa fursa ya kuwasilisha uzoefu wa nchi katika usimamizi wa uchumi, ukusanyaji wa rasilimali za ndani, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuharakisha maendeleo ya viwanda kwa kushirikiana na sekta binafsi, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu “Kufadhili Maendeleo ya Viwanda Barani Afrika kwa Maendeleo Endelevu.”

Related articles

Recent articles