33.7 C
New York

Majanga ya moto tishio maeneo ya starehe

Published:

BANGKOK, Thailand

TUKIO la baa kuwaka moto na kuua watu 27, sambamba na kujeruhi wengine kadhaa, mjini Bangkok, Thailand, limeteka vichwa vya habari duniani.

Wakati huo huo, ni mwendelezo wa maeneo ya starehe, zikiwamo kumbi za usiku, kukutwa na majanga hayo katika miaka ya hivi karibuni.

Tukio hilo la Baa ya Na Ladprao, Kaskazini mwa Bangkok, ni la pili nchini Thailand baada ya lile la watu 67 kupoteza maisha katika ukumbi wa starehe Siku ya sherehe za Mwaka Mpya 2009.

Hata hivyo, kile kinachoibua shaka juu ya hali ya usalama katika maeneo ya starehe ni kwamba Thailand si nchi pekee inayokumbana na matukio ya aina hiyo.

Januari, 2026, tukio la moto kuunguza baa ya Crans-Montana nchini Uswis lilisababisha vifo vya watu 41 na kujeruhi wengine zaidi ya 100.

Desemba, 2025, moto uliunguza ukumbi wa usiku katika Kijiji’ cha Arpora, Jimbo la Goa nchini India, na kusababisha vifo vya watu 25, wakiwamo wapishi na watalii.

Pia, Machi, 2025, huko Macedonia, moto uliunguza klabu ya usiku ya Pulse nchini Macedonia. Watu 63 walifariki na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa.

Tukio la aina hiyo liliwahi kutokea Aprili, 2024, mjini Istanbul, Uturuki, na kuua watu 29. Ni katika ukumbi wa usiku ulioko chini ya jengo lenye ghorofa 16.

Lipo pia tukio la Oktoba, 2023, huko Hispania katika Mji wa Murcia. Moto katika ukumbi wa starehe ulisababisha vifo vya watu 13.

Vilevile, moto uliozuka baada ya makundi mawili kupigana ndani ya ukumbi wa starehe ulisababisha vifo vya watu 19 mwaka 2022 katika Jimbo la Weet Papua nchini Indonesia.

Mifano ya majanga ya moto kwenye maeneo ya starehe ni mingi, ikihusisha pia matukio katika nchi za Nigeria, Marekani, Romania, Brazil, Urusi, China, Argentina na Uholanzi.

Kutokana na mfululizo wa matukio hayo, hoja ya kutilia shaka kiwango cha usalama katika maeneo ya aina hiyo, nayo imeibuka.

Je, maeneo ya starehe katika maeneo yako yana mazingira ya usalama kiasi gani kwa wateja wake?

Related articles

Recent articles