LOS ANGELES, Marekani
ZIMEIBUKA ripoti zinazodai kuwa kipa wa kimataifa wa Nigeria, Maduka Okoye, ‘anatoka’ na bibiye mwenye jina kubwa katika muziki wa Hip hop nchini Marekani, Cardi B.
Taarifa hizo zimevuma baada ya wawili hao kuonekana wakiwa na ukaribu mkubwa wakati wa Tamasha maarufu la mitindo nchini Ufaransa, Paris Fashion Week.
Katika video moja, Okoye anayeidakia Udinese ya Italia anaonekana akimkaribisha Cardi B kukaa naye karibuni, jambo ambalo bibiye huyo hakupinga.
Wakiwa jirani ukumbini hapo, walionekana wamezama kwenye stori, huku Cardi B akionekana mara zote kuwa ni mwenye furaha.
Aidha, taarifa za mastaa hao kuwa wapenzi zimekuja ikiwa ni miezi mitano tu imepita tangu Cardi B alipoachana na Stefon Diggs.
Cardi B na Diggs walibahatika kupata mtoto mmoja, ingawa tayari rapa huyo alikuwa na wengine watatu katika mahusiano yake ya kwanza na mwanamuziki mwenzake, Offset.
HUYU NDIYE OKOYE
Alizaliwa mwaka 1999 nchini Ujerumani anakotokea mama yake, huku baba akiwa ni raia wa Nigeria. Okoye ameamua kuitumikia ‘Super Eagles’.
Alijiunga na ‘academy’ ya Bayern Leverkusen mwaka 2009, kabla ya kuondoka miaka nane baadaye na kutua Fortuna Dusseldorf.
Tangu hapo, Okoye amezitumikia Sparta Rotterdam ya Uholanzi ambayo alikuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa klabu msimu wa 2020-21, Watford, kabla ya kusajiliwa Udinese mwaka 2023.
Julai, 2025, mlinda mlango huyo alifungiwa miezi miwili na Shirikisho la Soka la Italia kwa makosa ya upangaji wa matokeo katika mchezo wao dhidi ya Lazio.
Oktoba 13, 2019, alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na Super Eagles alipotokea benchi katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Brazil. Ilikuwa mechi ya kirafiki.


