LOS ANGELES, Marekani
WHATSAPP ni miongoni mwa mitandao ya kijamii yenye ushawishi mkubwa, ukitajwa kuwa na watumiaji zaidi ya bilioni tatu duniani kote.
Sasa, imezoeleka kuona usajili wa akaunti na matumizi ya WhatsApp kwa ujumla yakitegemea namba ya simu, siyo? Mabadiliko yanakuja.
Iko hivi; Kampuni ya Meta inayomiliki WhatsApp inakuja na utaratibu tofauti, ambapo utajisajili kwa kuweka jina la mtumiaji (username), badala ya namba ya simu kama ilivyo sasa.
Mfano rahisi, ni kama utaratibu unaokutana nao kwenye usajili wa akaunti ya Facebook au Instagram, ambapo unatakiwa kujaza jina unalotaka watu walitumie kukutafuta.
Meta wanaeleza kuwa hiyo ni moja ya hatua kubwa za kuboresha ulinzi na usalama wa taarifa za mtumiaji.
Kwamba mtumiaji atafikiwa na watu wanaolifahamu jina lake, tofauti na sasa, ambapo namba ya simu pekee inatosha hata kufikiwa na mtu asiyemfahamu.
Akifafanua zaidi, Makamu wa Rais wa Bidhaa wa WhatsApp, Alice Newton-Rex, amesema:
“Tumeweka hii kwa ajili ya usalama zaidi. Watu watatakiwa walijue jina sahihi unalotumia (username) ili kuwasiliana na wewe kwa mara ya kwanza.”
Aidha, ‘usernames’ itapaswa na herufi/alama zisizopungua tatu na zisizozidi 35. Pia, haitokuwa makosa kutumia username za mitandao mwingine ya Meta; Instagram na Facebook.
Hata hivyo, bado Meta hawajaweka rasmi ni lini utaratibu huo utaanza kufuatwa.


