MIAMI, Marekani
NI kama haikuwa na bahati. Baada ya sare dhidi ya New Zealand na Ubelgiji, timu ya soka ya Taifa ya Iran ilihitaji ushindi tu mbele ya Misri ili kuingia hatua ya 32 Bora ya msimu huu wa Kombe la Dunia.
Dhidi ya Misri, zilikuwepo dalili zote za Iran kusonga mbele. Misri walitangulia, kisha Iran wakasawazisha kupitia kwa Ramin Rezaeian.
Hata kabla ya Rezaeian, Iran ingeweza kupata bao la kusawazisha endapo Mehdi Taremi asingekosa mkwaju wa penalti.
Katika dakika za jioni (97), Misri haikuamini kilichotokea baada ya Iran kupata bao la pili, mfungaji akiwa ni Shoja Khalilzadeh.
Wakati dunia ikiona Iran imeshaingia hatua ya 32 Bora, mambo yaliwageukia baada ya VAR kulikataa bao hilo kwa madai ya ‘off-side’.
Kwa sare hiyo ya bao 1-1, Iran ilipaswa kusubiri matokeo ya mchezo kati ya Algeria na Austria ili kujua hatima yake ya kwenda 32 Bora au kuishia makundi.
Iran kusonga mbele ilitegemea timu yoyote ishinde. Sare haikuwa na faida kwa Taifa hilo la Kiarabu.
Baada ya muda mrefu wa sare ya mabao 2-2, Riyard Mahrez aliifungia Algeria bao la tatu dakika ya 93. Iran wakawa na matumaini makubwa.
Hata hivyo, katika dakika ya 96, Austria waliharibu mipango ya Iran baada ya kupata bao la kichwa kupitia kwa nyota wake, Sasa Kalajdzic. Iran ikawa hoi.
Lakini, mikosi haikuanzia hapo. Kombe la Dunia likiwa halijaanza, Marekani iliitangazia Iran kuwa itaingia nchini humo siku moja kabla ya mechi zake.
Kutokana na uhasimu wa kisiasa, timu ya soka ya Taifa ya Iran ilihamisha kambi yake kutoka Arizona, Marekani, hadi Tijuana, Mexico.
Kwamba hata baada ya kulegezewa na kuingia Marekani siku mbili kabla ya mechi, walikuwa wakirudi Mexico kila baada ya dakika 90 kumalizika.
Kocha wa Iran, Ghalenoei, anaamini Iran ndiyo timu pekee iliyoteseka kipindi hiki cha fainali za Kombe la Dunia.
“Walichokifanya wachezaji wangu kinapaswa kuandikwa katika historia kwa namna wenyeji walivyotufanyia,” alisema Ghalenoei.
“Licha ya matatizo yote hayo, tumeweza kuonesha kiwango kikubwa na dunia inajivunia Wairan na timu yetu.”


