27.3 C
New York

Huyu ndiye tapeli hatari zaidi sekta ya Afya

Published:

LOS ANGELES, Marekani

HIVI karibuni, Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI) lilimtia mkononi mfanyabiashara maarufu, Ibrahim Khaldoon Hilmi, aliyekuwa akikimbia kukamatwa kwa miaka mingi.

Khaldoom Hilmi aliyekamatwa akiwa Uturuki, anatajwa kujiingizia mabilioni ya fedha kwa njia za utapeli kwenye sekta ya afya nchini Marekani.

Tajiri huyo anatajwa kutengeneza mfumo wa utapeli kwenye Mfumo wa Bima ya Afya Medicare, ambao huwahudumia raia wenye umri wa kuanzia miaka 65 na vijana wenye ulemavu.

Katika mifumo yake, Khaldoon Hilmi ameweza kuvuna Dola za Marekani bilioni 3.7, huku Mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, akisema ni wizi mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika sekta ya afya.

Hilmi ni mfanyabiashara raia wa Marekani, ambaye makazi yake yako Florida. Alikuwa akiendesha kampuni kadhaa, ambazo usajili wake ulihusu biashara ya huduma za afya.

Miongoni mwa kampuni hizo ni Sunshine Senior Solutions, ambayo ilishinda zabuni ya Medicare katika eneo la kusambaza vifaa vya tiba kwa wazee.

Hata hivyo, kwa mujibu wa waendesha mashitaka, Hilmi alitumia ‘njia za panya’ kuvuna pesa kutoka Medicare, ikiwa ni pamoja na kughushi nyaraka ili alipwe.

Katika nyaraka hizo, ilikuja kubainika kuwa hakupeleka vifaa kwa baadhi ya wateja na aliongeza majina ‘feki’ ili kuvuna fedha zaidi.

Baada ya timu ya FBI kuanza uchunguzi, Hilmi aliamua kukimbia. Mei, 2025, kwa mujibu wa taarifa za FBI, aliondoka Marekani na tangu hapo akawa mtu wa kujificha ili kukwepa kudakwa.

Hata hivyo, mamlaka za Uturuki zilikuja kubaini kuwa mfanyabiashara huyo yuko nchini kwao, hivyo kuanza kumfuatilia, kisha kumdaka na kumkabidhi kwa FBI.

Aliwasili Marekani kwa ndege binafsi, ambapo picha zilimuonesha akiwa na pingu mikononi, tena chini ya ulinzi mkali wa maofisa wa FBI.

Aidha, kukamatwa kwa Hilmi kunakuja zikiwa ni wiki chache tu tangu FBI ilipomdaka na kumrejesha Marekani mshukiwa mwingine wa utapeli kwenye Mfumo wa Bima wa Medicare, Herbert Kimble.

Kwa upande wake, katika mazingira sawa na hayo ya Hilmi, Kimble anatajwa kujiingizia Dola bilioni 1.3 kutoka kwenye Mfumo huo. Kwa pamoja, wawili hao wamechota Dola bilioni 5.

Related articles

Recent articles