ROMA, Italia
KATIKA kipindi ambacho idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa duniani inaendelea kuongezeka kutokana na migogoro, mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kiuchumi, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, ametuma ujumbe mzito wa mshikamano kwa kutembelea makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) mjini Roma, Italia.
Ziara hiyo, iliyofanyika wiki hii, imeangazia umuhimu wa kuimarisha juhudi za kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa, wakati dunia ikikabiliwa na ongezeko la mahitaji ya msaada wa chakula kwa mamilioni ya watu walioathiriwa na vita, majanga ya tabianchi na misukosuko ya uchumi.
Akiwa ameandamana na viongozi wa WFP, Papa Leo XIV alianza ziara yake kwa kutembelea ukuta wa kumbukumbu ya wafanyakazi wa shirika hilo waliopoteza maisha wakiwa kazini katika maeneo ya migogoro na majanga. Papa aliweka shada la maua kuwakumbuka watumishi hao kabla ya kuzungumza na wajumbe wa bodi ya utendaji pamoja na wafanyakazi wa WFP kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Katika hotuba yake, Papa alisema njaa siyo tu janga la kibinadamu, bali pia ni tishio kwa amani, mshikamano wa kijamii na maendeleo ya dunia.
Alisema njaa hudhoofisha jamii, huongeza hatari ya migogoro na kuwalazimu watu kuhama makazi yao kwa sababu ya ukosefu wa mahitaji ya msingi ya maisha.
“Ni zaidi ya hofu ya masuala ya kibinadamu; njaa inamomonyoa mshikamano wa kijamii, inaongeza hatari za migogoro na kuchochea watu kufunga virago na kuhama makazi yao,” amesema Papa Leo XIV.
Kwa mujibu wa WFP, ziara hiyo imefanyika katika kipindi ambacho shirika hilo linakabiliwa na shinikizo kubwa la mahitaji ya misaada ya chakula duniani, huku changamoto ya upungufu wa fedha ikizidi kuwaathiri watu walio katika mazingira hatarishi zaidi.
Akizungumza na wafanyakazi wa WFP wanaotekeleza majukumu yao katika maeneo ya migogoro na majanga, Papa ametoa pongezi kwa kujitolea kwao kuokoa maisha ya watu na kuwafikia wale walio katika hali ngumu zaidi.
Aidha, alionya kuwa njaa huendeleza mzunguko wa udhaifu katika jamii na hatimaye kuathiri ustawi wa jumuiya nzima ya kimataifa, hivyo kusisitiza umuhimu wa mshikamano wa kweli wa dunia katika kutafuta suluhisho la kudumu dhidi ya tatizo hilo.
Ziara ya Papa Leo XIV katika makao makuu ya WFP imeonekana kuwa ishara ya matumaini, lakini pia wito wa wazi kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za pamoja kuhakikisha hakuna mtu anayelala njaa katika dunia yenye uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kwa kila mmoja.


