20.3 C
New York

Kisa maandamano, polisi Kenya wafunga njia kuu Nairobi

Published:

NAIROBI, Kenya

JIJI la Nairobi limeingia katika tahadhari kubwa ya kiusalama huku polisi wakiweka vizuizi katika barabara kuu na maeneo muhimu ya kuingia katikati ya jiji, kuelekea maandamano ya ukumbusho wa vuguvugu la Gen Z yanayotarajiwa kufanyika leo.

Hatua hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za usafiri jijini humo, baada ya matatu na magari mengine ya uchukuzi wa umma kuzuiwa kuingia katikati ya jiji, hali iliyosababisha msongamano mkubwa wa magari na kuwaacha mamia ya wasafiri wakikwama katika maeneo mbalimbali.

Maandamano hayo yanaandaliwa kuwakumbuka waathirika wa maandamano ya Juni 25, 2024, yaliyotikisa Kenya na kuandika ukurasa mpya katika historia ya harakati za kiraia nchini humo. Siku hiyo, waandamanaji waliingia katika majengo ya Bunge la Kenya wakipinga Mswada wa Fedha uliokuwa umependekeza nyongeza ya ushuru, hatua iliyochochea hasira kubwa miongoni mwa vijana.

Vijana hao, waliotambulika zaidi kama Gen Z, walitumia maandamano hayo kushinikiza uwajibikaji wa viongozi, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na mabadiliko ya kisiasa, huku baadhi yao wakitaka hata kuondolewa madarakani kwa Rais William Ruto na viongozi wengine wa serikali.

Katika kumbukumbu ya mwaka huu, baadhi ya Wakenya, wakiwemo manusura wa maandamano hayo, wanatarajiwa kushiriki maandamano ya kitaifa pamoja na shughuli za kuwasha mishumaa kwa ajili ya kuwaenzi waliopoteza maisha katika harakati hizo.

Licha ya kupita kwa miaka miwili tangu maandamano ya Juni 25, 2024, familia za takribani watu 19 waliouawa katika maandamano hayo bado zinaendelea kusubiri haki, huku madai ya uwajibikaji kwa waliotumia nguvu kupita kiasi yakibaki kuwa sehemu ya mjadala wa kitaifa.

Kumbukumbu za vuguvugu hilo pia zimeendelea kugubikwa na majonzi. Mwaka 2025, katika maadhimisho ya mwaka mmoja tangu maandamano hayo, watu wengine 16 waliripotiwa kufariki dunia kutokana na majeraha ya risasi na madhara yaliyohusishwa na matumizi ya nguvu ya polisi wakati wa kudhibiti waandamanaji.

Maandamano ya Gen Z sasa yanaonekana kuwa zaidi ya tukio la kupinga ushuru, bali alama ya kizazi kipya cha Wakenya wanaotaka uwazi, uwajibikaji na mabadiliko ya kweli katika uongozi wa nchi yao.

Related articles

Recent articles