Na Ramadhan Hassan, Gazetini-Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali itaendelea kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa haki ya kupata elimu, ikiwemo mabinti waliopata ujauzito, kama sehemu ya juhudi za kuimarisha usawa na ujumuishi katika sekta ya elimu nchini.
Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo leo Juni 16, 2026 jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, ambapo alisema siku hiyo ni kumbusho muhimu kwa jamii kuhusu wajibu wa kulinda na kuendeleza haki za watoto, pamoja na kuwakumbuka watoto wa Soweto nchini Afrika Kusini waliopigania haki ya kupata elimu bora.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuiweka elimu miongoni mwa vipaumbele vyake vya maendeleo, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga jamii yenye maarifa na ujuzi.
“Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa kila mtoto wa Kitanzania lazima apate elimu. Kwa msingi huo, Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha usawa na ujumuishi katika elimu kwa watoto wote,” alisema Prof. Mkenda.
Alibainisha kuwa juhudi hizo zinajumuisha kuimarisha usawa wa kijinsia na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuwanyima watoto fursa ya kujifunza na kutimiza ndoto zao.
“Hakuna mtoto atakayeachwa nyuma katika mfumo wa elimu. Hata mabinti waliopata ujauzito wanaruhusiwa na wanapaswa kurejea shuleni kuendelea na masomo yao,” alisisitiza.
Aidha, Waziri huyo alieleza umuhimu wa kuendelea kuboresha mazingira ya shule ili yawe salama na rafiki kwa watoto wote, jambo litakalowezesha wanafunzi kujifunza kwa ufanisi zaidi na kufikia malengo yao ya kielimu.
Prof. Mkenda pia alitoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini, mashirika mbalimbali na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda na kuendeleza haki za watoto.
Alisema ushirikiano huo unapaswa kuelekezwa katika kuhakikisha watoto wote wanapata huduma muhimu za msingi ikiwemo elimu bora, huduma za afya, maji safi na salama pamoja na mazingira bora ya kukua na kujiendeleza.
“Maendeleo ya taifa yanategemea namna tunavyowekeza kwa watoto wa leo. Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha watoto wanapata fursa stahiki za kukua, kujifunza na kutimiza ndoto zao,” alisema.


