Na mwandishi wetu, Gazetini
SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi ya OpenMap Development Tanzania (OMDTZ) imechukua hatua mpya za kuimarisha utayari wa jamii kukabiliana na mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuthibitisha mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika kata tano zinazokabiliwa na hatari hiyo.
Hatua hiyo imefikiwa kupitia warsha ya kupitia na kuthibitisha Mipango ya Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa kwa kata za Makurumula, Mabibo, Keko, Ubungo na Tabata, iliyowakutanisha viongozi wa serikali za mitaa, kamati za usimamizi wa maafa, wataalamu wa maafa na wadau mbalimbali.
Akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni za Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Selestine Masalamado, amesema mipango ya maafa inapaswa kuwa ya vitendo na inayoweza kutekelezeka ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Amesema mradi wa Ramani Zetu, Sauti Zetu unaofadhiliwa na Zayed Sustainability Prize kupitia OMDTZ na kutekelezwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu, umefika wakati muafaka katika kuimarisha usimamizi wa maafa nchini.
“Tunatarajia mradi huu utachangia kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na majanga mbalimbali, hususan mafuriko,” amesema Kanali Masalamado.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa OMDTZ, Innocent Maholi, amesema taasisi hiyo itaendelea kutumia teknolojia, uchoraji ramani shirikishi na mifumo ya tahadhari ya mapema kusaidia jamii zilizo katika maeneo hatarishi.
Naye Mratibu wa Maafa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Gerald Sondo, amesema katika miezi mitatu iliyopita kamati za maafa zimefanya tathmini ya vihatarishi, kubaini njia za uokoaji, maeneo salama na kuandaa mifumo ya mawasiliano ya dharura.
Amesema mipango hiyo itakuwa mwongozo muhimu kwa wananchi kabla, wakati na baada ya maafa, huku ikisaidia kupunguza athari za mafuriko na kuimarisha ustahimilivu wa jamii katika Jiji la Dar es Salaam.


