LONDON, Uingereza
SIKU zinazidi kusogea na sasa zimebaki tisa tu kabla ya filimbi ya kwanza kupulizwa msimu huu wa fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Juni 11, 2026, zikifanyika kwa mara ya kwanza katika nchi tatu (Marekani, Mexico na Canada).
Sasa, kwa kuangalia thamani ya wachezaji kwenye soko la usajili kupitia tovuti ya Transfermarkt, Ufaransa ndiyo timu ghali zaidi msimu huu wa mashindano.
Kwa wachezaji 26 walioitwa, Ufaransa inakwenda Kombe la Dunia ikiwa na timu yenye thamani ya Pauni bilioni 1.28.
Mbali na wengine, thamani hiyo inatokana na uwepo wa mastaa watatu; Kylian Mbappe (Pauni milioni 173.1), Michael Olise (Pauni milioni 129.8) na Ousmane Dembele (Pauni milioni 86.6).
England inashika nafasi ya pili kwa timu yake kuwa na thamani ya Pauni bilioni 1.13, licha ya kuwaacha Cole Palmer, Phil Foden na Trent Alexander-Arnold.
Katika nafasi ya tatu, ni timu ya Taifa ya Hispania, ambayo inakwenda kushiriki fainali za Kombe la Dunia ikiwa na thamani ya Pauni bilioni 1.1, ikifuatiwa na Ujerumani (Pauni mil. 880) na Ureno (Pauni mil. 828.4).


