CAIRO, Misri
MKONGWE wa soka la Brazil, Pele, aliwahi kutabiri kuwa siku moja Kombe la Dunia litatua Afrika. Alisema hilo lingetokea mwaka 2000. Isivyo habari, haikutokea hadi anafariki.
Msimu uliopita, 2022, Afrika ilipiga hatua kubwa baada ya Morocco kuwa timu ya kwanza barani Afrika kufika nusu fainali ya michuano hiyo.
Safari hii, katika fainali za mwaka huu zitakazoanza Juni 11, 2026, Afrika itakuwa na wawakilishi 10 kati ya ya timu 48 zitakazoshiriki.
Brazilian great Pelé famously said he believed an African side would win the World Cup by the year 2000. That has not happened, but Morocco’s form and the excellence shown by the likes of Senegal and Ivory Coast in recent years suggest teams are getting closer
MOROCCO ilifika nusu fainali msimu uliopita wa fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar na kuandika historia ya kuwa mwakilishi pekee wa Afrika kufika hatua hiyo.
Safari hii, Afrika itakuwa na wawakilishi 10 kati ya mataifa 48 yanayoshiriki michuano hiyo itakayoanza Juni 11, 2026.
Je, ni wakati wa Afrika kuwa na matumaini ya kubeba Kombe hilo msimu huu na kutimiza ndoto ya lejendari Pele?
ALGERIA
Inashika nafasi ya 28 katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la mchezo huo duniani (FIFA). Kocha wao ni raia wa Bosnia-Herzegovina, Vladimir Petkovic.
Algeria wanarejea Kombe la Dunia baada ya kuikosa kwa misimu miwili mfululizo (2018 na 2022) na wako kundi moja na Argentina, Jordan na Austria. Watawavaa akina Lionel Messi katika mechi ya kwanza itakayochezwa Juni 16.
CAPE VERDE
Nafasi ya 69 katika viwango vya FIFA. Kocha ni Bubista na wako kundi moja na Hispania, Uruguay na Saudi Arabia.
Ni mara yao ya kwanza kucheza Kombe la Dunia na walifuzu kwa kuinyima tiketi Cameroon. Wachezaji wake wengi wanacheza soka la kulipwa nchini Ureno.
DRC
Nafasi ya 46 katika viwango vya FIFA na kikosi chake kinanolewa na kocha raia wa Ufaransa, Sebastien Desabre.
DRC wanarejea kwa mara ya kwanza baada ya kukosekana Kombe la Dunia tangu mwaka 1974. Wako kundi moja na Ureno watakaoanza nao Juni 17, Colombia na Uzbekistan.
MISRI
Nafasi ya 29 katika viwango vya FIFA na kocha ni mshambuliaji wao wa zamani, Hossam Hassan. Mafarao wako kundi moja na Ubelgiji watakaoanza nao Juni 15, New Zealand na Iran.
Tumaini la Wamisri lipo kwa nyota wake wawili wanaofanya vizuri barani Ulaya, Mohamed Salah na Omar Marmoush.
GHANA
Nafasi ya 74 kwenye viwango vya FIFA. Kocha ni raia wa Ureno, Carlos Queiroz. Ghana imekuwa kwenye kiwango kisichoridhisha kwa miaka ya hivi karibuni, ikishindwa hata kufuzu AFCON 2025.
Wako kundi moja na Panama watakaoanza nao Juni 17, England na Croatia. Ni mtihani mkubwa kwao, ikizingatiwa kuwa ni timu mbili pekee zitakazovuka makundi.
IVORY COAST
Nafasi ya 34 kwenye viwango vya FIFA na kocha ni Emerse Fae. Wamerejea baada ya kukosekana Kombe la Dunia kwa miaka 12.
Mabingwa hao wa AFCON 2023 wako kundi moja na Ecuador watakaoanza nao Juni 14, Ujerumani na Curacao.
MOROCCO
Nafasi ya nane kwenye viwango vya FIFA na kocha ni Mohamed Ouahbi aliyechukua nafasi ya Walid Regragui aliyewafikisha nusu fainali mwaka 2022.
Morocco wako kundi moja na Brazil, Scotland na Haiti. Wataanza na Wabrazil katika mchezo utakaochezwa Juni 13.
SENEGAL
Nafasi ya 14 kwenye viwango vya FIFA na kocha ni Pape Thiaw. Ni moja ya timu za Afrika zenye nafasi kubwa ya kufanya vizuri.
‘Simba wa Teranga’ wako kundi moja na Ufaransa watakaoanza nao Juni 16, Norway na Iraq. Je, watavuka kundi hilo?
AFRIKA KUSINI
Nafasi ya 60 kwenye viwango vya ubora duniani. Kocha wao ni raia wa Ubelgiji, Hugo Broos. Bafana Bafana wanashiriki kwa mara ya kwanza tangu walipokuwa wenyeji mwaka 2010.
Wako kwenye kundi gumu, ambalo lina Mexico watakaoanza nao Juni 11, Jamhuri ya Czech na Korea Kusini. Bafana Bafana watatoboa?
TUNISIA
Nafasi ya 44 duniani. Kocha ni Sabri Lamouchi na Tunisia iko kundi moja na Sweden watakaoanza nao Juni 14, Japan na Uholanzi.
Tunisia inashiriki kwa mara ya sita katika misimu nane ya Kombe la Dunia ya hivi karibuni. Je, watavuka makundi kwa mara ya kwanza?


