NYON, Uswis
NI siku chache tu zimebaki kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia, ambazo kwa mara ya kwanza zitafanyika katika nchi tatu tofauti; Marekani, Mexico na Canada.
Kuelekea fainali hizo, zipo sheria na kanuni mpya zilizotambulishwa Februari, 2026, na Bodi ya Chama cha Soka cha Kimataifa (IFAB).
Kwa mujibu wa IFAB, muongozo huo utaanzia Kombe la Dunia, kisha utatumika katika michuano yote ya kimataifa.
Mosi, mwamuzi atahakikisha hazizidi sekunde tano katika tukio la kurusha mpira, kona au ‘goal kick’ (kipa kupiga mpira).
Endapo zitavuka sekunde hizo bila kitendo kufanyika, mathalan pigo la kona, mwamuzi ataamuru timu pinzani kupewa nafasi hiyo.
Pili, mchezaji aliyefanyiwa mabadiliko, kwa maana ya kuitwa benchi, atatakiwa awe ametoka uwanjani ndani ya sekunde 10.
Endapo atachelewa katika muda huo, mwamuzi ataamuru mchezo uendelee na mchezaji anayetakiwa kuingia atasubiri hadi utakaposimama tena.
Tatu, mchezaji yeyote (isipokuwa kipa) atapatiwa matibabu nje ya uwanja. Lakini, hii haimuhusu aliyeumia kwa rafu illyosabaisha kadi kwa mpinzani.
Nne, mchezaji mwenye kadi za njano mbili katika michezo tofauti atakosa mechi moja lakini zitafutwa zote baada ya hatua ya makundi kumalizika. Awali, ziliendelea kuhesabiwa hadi robo fainali.
Tano, itakuwa ni adhabu ya kadi nyekundu kwa mchezaji kunaswa akiziba mdogo wakati wa mazungumzo, ikitafsiriwa kuwa huenda alitukana au kutoa kauli za kibaguzi.
Sita, kadi nyekundu itawahusu wachezaji wote watakaotoka nje ya uwanja kama njia ya kugomea maamuzi ya refa.


