TEHRAN, Iran
MAREKANI inaitaja Iran kama mfadhili wa vikundi vyote vya kigaidi vilivyopo Mashariki ya Kati. Kwamba tangu ilipofanya mapinduzi mwaka 1979, imekuwa chanzo cha ugaidi katika Ukanda huo.
Marekani kuihusisha Iran na ugaidi haikuanza leo, jana wala juzi. Ni tangu mwaka 1984, ndipo kwa mara ya kwanza Marekani ilisema Iran inafadhili ugaidi Mashariki ya Kati.
Madai ya Marekani ni kwamba Iran imekuwa ikiwapa magaidi, wakiwamo wa Hezbollah nchini Lebanon, msaada wa silaha, fedha na hata mafunzo, lengo likiwa ni kuviwezesha kuleta mapinduzi ya Kiislam katika nchi zao (Bahrain, Iraq, Lebanon, Palestina, Syria na Yemen).

Mbali ya Hezbollah, ambao Marekani inadai kuwa Iran iliwapa msaada wa Dola milioni 700 kwa mwaka 2020 pekee, Kundi jingine la kigaidi la Mashariki ya Kati linalohusishwa na Iran ni Hamas la Palestina.
Baada ya Marekani kwa kushirikiana na Israel kuanza kushambulia Iran (Februari 28, 2026), Hezbollah na Hamas viliibuka na kuanza kulisaidia Taifa hilo la Kiarabu.
Kama hiyo haitoshi, viliibuka vikundi vingine kuingilia vita hivyo, wakiwamo Houthis wa Yemen na ‘Harakat Ashab al-Yamin al-Islamiyya’, hiyo ikithibitisha kile kilichoelezwa juu ya ufadhili wanaopewa na Iran.
Kwa pamoja, makundi hayo yamekuwa yakiishambulia Marekani, Israel na washirika wao wa Ukanda wa Mashariki ya Kati.
Mathalan, hao wanaoitwa Harakat Ashab al-Yamin al-Islamiyya walikiri kutekeleza mashambulizi mengi ya Machi-Aprili, 2026, dhidi ya jamii ya Wayahudi katika nchi za Uholanzi, Ubelgiji na Uingereza.
HEZBOLLAH
Ni jina la Kiarabu lenye maana ya ‘Chama cha Mungu’. Ni Kundi lililoanzishwa miaka ya 1980 na Wasilam wa Dhehebu la Shia, wakati Lebanon ikiwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwanzoni mwa maisha ya Kundi, Hezbollah walihusika katika shambulizi la bomu kwenye ubalozi wa Marekani mjini Beirut mwaka 1984, ambapo watu 63, wakiwamo raia wa Marekani 17, walipoteza maisha.
Mwaka 1992, Hezbollah walishambulia kwa bomu Ubalozi wa Israel mjini Buenos Aires, Argentina, na kuua watu 29 na kujeruhi 242, kuharibu Kanisa Katoliki, shule na nyumba ya kulelea wazee.
Pia, walishambulia Kituo cha AMIA mjini Buenos Aires mwaka 1994 na kuua watu 85, achilia mbali kulipiga bomu basi la watalii wa Israel waliokuwa nchini Bulgaria mwaka 2012.
Moja ya malengo yake ni kuliondosha katika uso wa dunia Taifa la Israel. Licha ya kuwa Mashariki ya Kati, ni Kundi lenye mtandao mkubwa Ulaya, Amerika na hata Afrika.
HAMAS
Jina lao jingine ni Islamic Resistance Movement. Ni Kundi lililoanzishwa mwaka 1988 na limekuwa likipigania kile kinachoelezwa kuwa ni masilahi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Uhusiano wake na Iran umekuwa wa kupanda na kushika. Mathalan, mwaka 2012, Iran ilisitisha misaada baada ya Hamas kukataa kuusaidia utawala wa Rais Bashir al-Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.
Mwaka 2017, Hamas kupitia kwa viongozi waandamizi, Yahya Sinwar, ilitangaza kuwa uhusiano wake na Iran umekaa sawa na sasa wanapokea misaada kutoka kwa washirika wao.
Oktoba 7, 2023, Hamas walitekeleza shambulizi kubwa zaidi kuwahi kutokea dhidi ya Israel na kuua watu zaidi ya 12,00, wakiwamo raia wa Marekani, na kujeruhi wengine zaidi ya 5,400. Pia, Kundi hilo liliteka watu zaidi ya 250.
Israel ilifanikiwa kuwaua viongozi kadhaa wa Hamas, wakiwamo Yahya Sinwar, Mohammed Deif, Marwan Issa, Mohammed Sinwar (kaka wa Yahya), na Ismail Haniyeh.
Kwa sasa, Kundi linaongozwa na Ezzedin al-Haddad, ambaye jina lake maarufu ni ‘Mzimu’ kutokana na mitego kadhaa ya kuuawa aliyowahi kuiruka.


