12.9 C
New York

Nini ufanye, uepuke wakati wa Sikukuu ya Kuchinja?

Published:

Na Hassan Mwasha

MEI 27, 2026, waumini wa Dini ya Uislam wa Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar wataungana na wenzao duniani kote kusherehekea Sikukuu ya ‘Al-Adha’.

Wengi wanaifahamu kwa jina la ‘Sikukuu ya Kuchinja’ kutokana na asili yake, kwa mujibu wa mafundisho ya Kitabu Kitakatifu cha Qur-an.

Ni Sikukuu inayoadhimishwa mara moja kwa mwaka, tena siku ya mwisho ya kumalizika kwa Ibada ya Hijja mjini Makkah, Saudi Arabia.

Kwa mwaka huu, licha ya hali tete ya usalama katika eneo la Mashariki ya Kati, waumini zaidi ya milioni 1.5 wamefika Makkah kutekeleza nguzo hiyo ya mwisho kati ya zile tano za Uislam.

Aidha, ieleweke kuwa Sikukuu ya ‘Al-Adha’ husherehewa katika siku ya 10 ya mwezi wa 12 (Dhul-Hijja) katika kalenda ya Kiislam.

Msingi wa jina la Sikukuu ya Kuchinja unatokana na kisa cha Nabii Ibrahim na mtoto wake wa kiume, alipopokea maagizo (kutoka kwa Mungu) kwamba amtoe sadaka kwa kumchinja.

Likiwa ni jaribio la kupimwa imani, Nabii huyo alifaulu kwani alikaribia kutekeleza maagizo hayo, na ndipo Mungu alipomzuia na kumpatia mnyama (kondoo) ili kumchinja.

Hivyo, katika kuenzi kile alichokifanya Nabii Ibrahim, Waislam duniani kote wamekuwa wakisherehekea Sikukuu hiyo kwa kuchinja mnyama/wanyama kwa ajili ya kula na kutoa sadaka kwa makundi maalumu.

Hata hivyo, wanyama wanaogusiwa hapo si pamoja na nguruwe na wale waliokatazwa katika Qur-an na mafundisho ya hadithi za Mtume Mohamed (s.a.w.).

Na badala yake, inahimizwa zaidi uchinjaji wa wanyama maarufu wa kufugwa, wakiwamo ng’ombe, mbuzi, kondoo na ngamia.

Mafundisho yanafafanua zaidi, kwamba inafaa zaidi kwa matumizi ya mnyama aliyechinjwa kugawiwa katika sehemu tatu; familia, ndugu/jamaa/marafiki, na watu wenye uhitaji katika jamii, wakiwamo yatima.

Kama zilivyo kwa Sikukuu zote, kwa mujibu wa Dini ya Uislam, ni haramu kujihusisha na vitendo viovu, ikiwamo unywaji wa pombe au zinaa wakati wa Sikukuu ya Kuchinja.

Na badala yake, muumini anapaswa kutumia Sikukuu hiyo kujikurubisha (kujisogeza) zaidi kwa Mungu, ikiwa ni pamoja na kuomba kusamehewa dhambi, kuepushwa na mabalaa na kuongezewa neema (riziki, afya, n.k.).

Related articles

Recent articles