26.5 C
New York

Argentina kupindua historia Kombe la Dunia 2026?

Published:

LONDON, Uingereza
TIMU ya Taifa ya Argentina itakwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu ikiwa bingwa mtetezi wa michuano hiyo baada ya kubeba ‘ndoo’ mwaka 2022 nchini Qatar.
Argentina chini ya kocha mzawa, Lionel Scaloni, inafukuzia rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutetea ubingwa tangu Brazil ilipofanya hivyo mwaka 1958 na 1962.
Tayari Scaloni ameshaita kikosi cha awali cha wachezaji 55, akiwamo Lionel Messi ambaye ndiye nahodha, akitarajiwa kushiriki kwa mara ya sita fainali hizo za Kombe la Dunia.
Watacheza mechi yao ya kwanza Juni 16, 2026 kwa kuivaa Algeria, kabla ya kukutana na Austria na Jordan katika Kundi J.
MASTAA KIBAO
Argentina ni moja ya mataifa yenye historia ya kuzalisha vipaji vikubwa vya soka vinavyotamba katika Ligi kubwa barani Ulaya.
Safari hii, miongoni mwa nyota walioitwa ni Emiliano Martinez (Aston Villa), Lisandro Martinez (Man United), Cristian Romero (Tottenham), na Enzo Fernandez (Chelsea).
Wengine ni Alexis Mac Allister (Liverpool), na Julian Alvarez (Atletico Madrid), Alejandro Garnacho (Chelsea), Lautaro Martinez (Inter), Giuliano Simeone (Atletico Madrid), na Matis Soule (Roma).
HIKI HAPA KIKOSI CHA KWANZA
Kikosi cha awali kina nyota 55 lakini kocha Scaloni atalazimika kubaki na 26 tu watakaopanda ndege kwenda Kombe la Dunia.
Katika mfumo wake wa 4-4-2 au 4-3-3, Scaloni anatazamiwa kuwatumia Thiago Almada, Julian Alvarez na Messi kwenye eneo la mwisho (ushambuliaji).
Ukija kwenye kiungo, ni wazi atachagua kuwatumia Enzo Fernandez, Leandro Paredes na Alexis Mac Allister.
‘Pacha’ ya eneo la beki wa kati inatarajiwa kuwa na Cristian Romero na Nicolas Otamendi, licha ya uwepo wa Lisandro Martinez na Marcos Senesi.
Kwa eneo la beki wa pembeni, ni Nahuel Molina na Nicolas Tagliafico, wakati golini akisimama Martinez wa Aston Villa kama ilivyokuwa wakati wa fainali zilizopita.

Related articles

Recent articles