WASHINGTON, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump amesema hakuwahi kutangaza kumalizika kwa operesheni za kijeshi dhidi ya Iran bali alieleza kuwa Marekani imefanikiwa kuishinda Iran katika mapambano ya kijeshi.
Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya Marekani ya ABC, Trump amesema Marekani haiwezi kuruhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia kutokana na kile alichodai kuwa ni misimamo hatari ya taifa hilo.
“Hatuwezi kuiruhusu Iran kuwa na silaha za nyuklia kwa sababu ni watu wenye misimamo hatari. Hatuwezi kuwaruhusu wapate uwezo wa nyuklia,” amesema Trump.
Alipoulizwa kama operesheni za kijeshi zimefikia mwisho, Trump alifafanua kuwa ushindi wa kivita hauumaanishi vita vimekwisha kabisa.
“Sikusema hivyo. Nilisema tumewashinda, lakini hiyo haimaanishi kuwa kila kitu kimeisha. Tunaweza kuendelea kwa wiki nyingine mbili na kushambulia malengo yoyote,” amesema.
Trump ameongeza kuwa baadhi ya malengo tayari yameshambuliwa kwa kiwango kikubwa huku akidai kuwa hata kama Marekani haitafanya mashambulizi mengine, Iran itahitaji miaka mingi kujijenga upya baada ya madhara yaliyosababishwa na mashambulizi hayo.


