Na mwandishi wetu, Gazetini
TANZANIA imepiga hatua kubwa katika kupunguza athari za malaria, huku takwimu za hivi karibuni zikionyesha kupungua kwa vifo, maambukizi na wagonjwa wa ugonjwa huo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, vifo vya malaria vimeshuka kwa asilimia 50 kutoka watu 2,460 mwaka 2020 hadi 1,231 mwaka 2025. Aidha, kiwango cha maambukizi katika jamii kimepungua kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022 hadi asilimia 5.7 mwaka 2025, sawa na upungufu wa karibu asilimia 30.
Takwimu hizo pia zinaonyesha idadi ya wagonjwa wanaogundulika na malaria katika vituo vya afya imeporomoka kutoka milioni 6 mwaka 2020 hadi milioni 2.8 mwaka 2025, huku wagonjwa wanaolazwa hospitalini kutokana na malaria wakipungua kwa asilimia 35.
Serikali imeeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa katika kudhibiti ugonjwa huo, ikiwemo kutenga Sh20 bilioni kwa miaka ya fedha 2024/25 na 2025/26 kwa ajili ya unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu.

Kupitia fedha hizo, lita 1,250,000 za viuadudu zimenunuliwa na kusambazwa katika halmashauri zote 184 nchini kama sehemu ya kuimarisha kinga dhidi ya malaria.
Pamoja na mafanikio hayo, Serikali imezindua Mpango Mkakati wa Taifa wa Malaria wa 2026–2030 wenye lengo la kuharakisha jitihada za kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Wataalamu wa afya wanasema ingawa mafanikio hayo yanatia matumaini, bado ushiriki wa jamii katika kutumia vyandarua, kuondoa mazalia ya mbu na kuwahi kupima dalili za malaria ni muhimu ili kufanikisha lengo la Tanzania kuwa huru dhidi ya malaria.


