34.9 C
New York

Ujerumani bado majanga Kombe la Dunia

Published:

MIAMI, Ujerumani

NUKSI ya timu ya soka ya Taifa ya Ujerumani katika fainali za Kombe la Dunia imeendelea. Safari hii, waliishia hatua ya 32 Bora.

Ni kwa msimu wa tatu mfululizo, Ujerumani imeshindwa kuingia hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Mara yao ya mwisho kuvuka hatua ya 16 Bora ilikuwa mwaka 2014, ambapo waliweza pia kutwaa ubingwa wakiwa nchini Brazil.

Msimu huu, safari yao ilikwamia hatua ya 32 Bora, tena mbele ya Paraguay, iliyowafunga kwa penalti 4-3 baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya uwanja.

Katika mchezo huo, waliokosa mikwaju yao ya penalti kwa upande wa Ujerumani ni Kai Havertz, Nick Woltemade na Jonathan Tah.

Hiyo ikawa mara ya kwanza kwa Ujerumani kupoteza kwa mikwaju ya penalti katika michuano ya Kombe la Dunia. Ilishinda mara nne kwa staili hiyo kabla ya kukutana na Paraguay.

Havertz alipoulizwa kama Ujerumani haipo tena katika zile timu kubwa duniani, alikiri kwa kusema ndiyo. “Ni wazi iko hivyo,” alisisitiza.

Wachambuzi wa soka nchini Ujerumani wanataja sababu za anguko la timu hiyo msimu huu wa Kombe la Dunia, wakianza kwa kuwatupia lawama wachezaji wakubwa kikosini.

Kwamba baadhi ya mastaa, wakiwamo Joshua Kimmich, Florian Wirtz na Jamal Musiala, hawakuonesha viwango vyao bora katika mechi zote nne walizocheza.

Wakati huo huo, wachambuzi wanaona wimbi la majeraha lilivyoigharimu timu hiyo, ikiwa ni pamoja na kuumia kwa Serge Gnabry na Lennart Karl kabla ya michuano kuanza.

Hata baada ya michuano kuanza, beki wao anayecheza Borussia Dortmund, Nico Schlotterbeck, alipata majeraha ya kumuweka nje mwezi mmoja. Aliumia katika mechi yao dhidi ya Ivory Coast.

Related articles

Recent articles