LAGOS, Nigeria
SUPASTAA wa muziki wa Nigeria, David Adeleke ‘Davido’, amefunguka mengi juu ya safari ya mafanikio yake katika sanaa hiyo.
Miongoni mwa aliyoyayasema ni kwamba kwa sasa hazitazami tuzo za Grammy kama alama ya mafanikio kwani ameshazizoea, tofauti na wakati ule anaanza muziki.
Katika mahojiano yake nchini Uingereza, Davido amesema amepata mafanikio makubwa kimataifa, hivyo haoni tena kama tuzo za Grammy ni kitu cha msingi sana kukipigania.
Mbali ya kutumbuiza katika mataifa mengi duniani, ikiwamo Marekani, Davido ametajwa mara mbili katika kuziwania tuzo hizo kwa miaka mitatu tu ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wake, akili yake kwa sasa ni kutengeneza muziki wenye vionjo vya Afrika, badala ya kutaka kuwavutia ‘wazungu’.
Katika hatua nyingine, Davido amejivunia ukubwa wa jina lake nchini Afrika Kusini akisema asilimia 80 ya raia wa nchi hiyo ni mashabiki wake.


