Na mwandishi wetu, Gazetini
SIKU chache baada ya kutoka sare ya kutokufungana dhidi ya Simba, Yanga imeibuka na kuitwanga barua nzito Kamati ya Uendeshaji ya Bodi ya Ligi (TPLB).
Yanga ioikuwa mwenyeji wa mchezo huo wa Mei Mosi, 2026 wa Ligi Kuu Bara uliochezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Sasa, katika barua yao ya leo Machi 7, 2026 Yanga imehitaji ufafanuzi wa mambo matano kutoka kwa TPLB.
“Tumelazimika kufanya hivyo kwa vile wanachama wao wanahitaji ufafanuzi wa mambo hayo,” amesema Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe.
Akifafanua, Kamwe amesema jambo la kwanza ni adhabu ya mshambuliaji wa Simba, Selemani Mwalimu, aliyefungiwa mechi tatu kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Dodoma Jiji.
“Yanga imetaka ufafanuzi wa kwa nini Kamati imetumia kanuni tofauti ya 41:5(5.2) iliyomfungia mechi tatu badala ya kutumika kanuni ya 41:21 ambayo ingefanya afungiwe mechi tano,” amesema.
Aidha, pia Yanga wametaka ufafanuzi juu ya kuchelewa kwa Kamati hiyo kutoa uamuzi wa suala la mshambuliaji huyo.
“Jambo la tatu ni ufafanuzi wa adhabu tofauti ambazo marefa wasaidizi wawili wa mechi baina yetu na Simba, kwa kosa moja la kushindwa kutafsiri sheria ya kuotea.
“Jambo la nne ambalo tunahitaji ufafanuzi wake ni la taarifa ya TPLB kudai refa msaidizi alikataa bao halali la Simba kinyume na muongozo wa sheria na taratibu za soka duniani.
Kamwe amesema kwa mujibu wa sheria za FIFA, bao halali ni lile goli pekee ambalo limeruhusiwa na mwamuzi wa kati.
“Kinyume na hapo hakuna kamati wala sheria au kanuni ambayo inayo mamlaka ya kuhalalisha goli ambalo halikuidhinishwa na mwamuzi wa kati.
“Kauli ya kwamba Simba wamenyimwa goli halali imeleta taharuki kwa umma. Tumeiandikia kamati itueleze imetoa wapi mamlaka ya kutangazia Uumma kuwa goli ni halali,” amesema Kamwe.
Akihitimisha, Kamwe amesema jambo la tano ni ufafanuzi wa kutoadhibiwa kwa refa msaidizi aliyeruhusu bao la pili la Simba dhidi ya KMC, Yanga ikidai kuwa bao hilo lililofungwa na Mwalimu lilikuwa la kuotea.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda, amesema itafuata taratibu za kikanuni katika kushughulikia suala hilo.
“Kikanuni klabu inaweza kuomba mrejesho kwa kamati hivyo Bodi kwa sasa haiwezi kuzijibu kwa vile zimeelekezwa kwa kamati ambayo bado haijakutana,” amesema Boimanda.


