MADRID, Hispania
NI tofauti ya pointi mbili tu. Real Madrid wako kileleni mwa msimamo, wakati Barcelona wako nyuma yao wakiwa na pointi 58, huku kila timu ikiwa imebakiza mechi 14.
Atletico Madrid ya kocha Diego Simeone, kama ilivyo Villarreal, iko nafasi ya tatu ikizidiwa pointi 15 na Madrid.
Kwa hesabu hizo, ni rahisi kubashiri kuwa ubingwa wa La Liga kwa msimu huu wa 2025-26 utaelekea Madrid au Barcelona.
Kwamba ni mwendelezo wa ubabe wao kwenye Ligi, ambapo timu hizo zimepokezana kombe kwa misimu 18 kati ya 20 ya hivi karibuni.
Madrid iko kwenye kiwango bora safari hii kwani imekusanya pointi 60 katika mechi 24 ilizoshuka dimbani.
Endapo watamaliza wakiwa na pointi 95, basi watakuwa wameifikia idadi waliyokuwa nayo walipotwaa ubingwa wa La Liga msimu wa 2023-24.
Kwa upande wa Barcelona, endapo watamaliza wakiwa na pointi 92, basi watakuwa wameifikia idadi kubwa zaidi kuwahi kuwa nayo tangu msimu wa 2017-18.
Aidha, Madrid na Barcelona zitakapokutana katika El Clasico ya Mei, 2026 zinatarajiwa kutoa picha halisi ya ubingwa wa msimu huu.


