Na Mwandishi Wetu, Gazetini
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amewataka wafanyabiashara wa vyakula nchini kuacha kuwaumiza wananchi katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma kwa kuongeza bei ya bidhaa kwa kisingizio cha upungufu wa chakula.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma leo Januari 29, 2029, wakati wa Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu amesema kuwa licha ya tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uhaba wa mvua, nchi haina uhaba wa chakula na kuna ziada ya kutosha.
Dk. Mwigulu amesema pia kuwa serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kusambaza chakula katika maeneo yenye uhitaji ili kuhakikisha Watanzania wanapata chakula cha kutosha.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Nancy Nyalusu, aliyetaka kufahamu mipango ya serikali katika kuhakikisha uhaba wa chakula haujitokezi wakati wa mfungo wa Kwaresma na Ramadhani.
“Kwa sasa tunachakula cha kutosha, mahitaji ya chakula cha akiba kwa nchi ni takribani tani 150,000 na sasa nchi ina zaidi ya tani 400,000 za akiba ya chakula rai ambayo niliitoa hata nilipokutana na wakuu wa mikoa ni kuendelea kuwahamasisha wananchi kuzingatia ushauri wa aina ya mazao ya kupanda.”
Pia, Waziri Mkuu amewaelekeza Wakuu wa Mikoa yote nchini wawaelimishe wananchi kuendelea kutumia vizuri chakula walichonacho kutokana na tahadhari ya upungufu wa mvua iliyotolewa na TMA.


