LONDON, Uingereza
MSIMU wa Ligi Kuu ya England (EPL) umeshuhudia teknolojia ya VAR ikifanya makosa mengi, hivyo kuwaingiza ‘chaka’ waamuzi na kuzigharimu timu mbalimbali.
Kwa mujibu wa BBC Sport, makosa ya VAR yamekuwa yakiongezeka kwa asilimia 30 kutoka msimu mmoja na mwingine, licha ya kwamba ujio wake ulilenga kuwasaidia waamuzi.
Kwa msimu wa 2022-23, teknolojia hiyo ilifanya makosa 23 na tayari imeshafanya hivyo mara 20 kufikia hatua hii ya msimu huu wa 2025-26.
Mosi, katika mchezo ambao Liverpool waliifunga Bournemouth mabao 4-2, kama VAR ingemsaidia mwamuzi wa kati, basi Senesi angelimwa kadi nyekundu kwa kitendo chake cha kuzuia kwa mkono mpira uliokuwa ukielekea kwa Hugo Ekitike.
Pili, katika mchezo kati ya Chelsea na Fulham, ambao Blues walishinda mabao 2-0, VAR ikifanya kosa la kukataa bao halali la Josh King, ingawa mwamuzi wa kati alishalikubali.
Tatu, katika mchezo ambao Wolves walifungwa mabao 3-2 na Everton, Hugo Beuno alifunga bao halali dakika ya 70 lakini VAR ililikataa.
Nne, wakati Brentford ikiifunga Manchester United mabao 3-1, kama si VAR, basi Nathan Collins alipaswa kulimwa kadi nyekundu kwa kitendo chake cha kumvuta jezi Bryan Mbeumo.
Tano, VAR ilifanya kosa jingine katika mchezo wa sare ya mabao 3-3 kati ya Crystal Palace na Bournemouth. Kama si VAR, basi Senesi angelimwa kadi nyekundu kwa rafu aliyomchezea Ismaila Sarr.


