LONDON, Uingereza
ALIKUWA na mchango mkubwa wakati Liverpool ilipokuwa ya moto chini ya kocha wa kimataifa wa Ujerumani, Jurgen Klopp.
Liverpool iliyotwaa taji la Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kulikosa kwa miaka 30. Liverpool iliyobeba ‘ndoo’ ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Anaitwa Thomas Gronnemark. Mtaalamu wa mipira ya kurusha, ambaye alimfanya beki wa pembeni, Andy Robertson, kuwa tishio katika kazi hiyo.
Arsenal, ambao wanasaka taji lao la kwanza la Ligi Kuu ya England (EPL) tangu walipolibeba msimu wa 2003-04, wamempa ajira kocha huyo wa kimataifa wa Denmark.
Akiwa mchezaji miaka mingi iliyopita, Gronnemark alikuwa hatari kwa mipira ya kurusha, ikiwa ni pamoja na kuweka rekodi ya dunia baada ya kurusha umbali wa meta 51.
Tangu alipostaafu, amekuwa akiajiriwa kuwanoa wachezaji, hasa mabeki, mbinu za kurusha mipira inayoweza kutengeneza nafasi za kufunga mabao.
Alifanya kazi hiyo akiwa na Brentford, Borussia Dortmund, Ajax, FC Midtjylland, Union Saint-Gilloise na JEF United ya Japan, hadi Klopp alipomvuta Anfield mwaka 2018.


