9.8 C
New York

Afrika imejifunza nini kilichomkuta Maduro?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MAREKANI kuishambulia Venezuela na kuondoka na Rais wake, Nicolas Maduro, ndiyo habari iliyogonga vichwa vya habari duniani kote kwa sasa.

Vikosi vya kijeshi vya Marekani vilimnyakua Maduro na mkewe, Cilia Flores, kisha kuwafungulia mashitaka mjini New York.

Kwa muda mrefu, Marekani imekuwa ikimshutumu Maduro kwa kile inachodai anaiongoza Vanezuela kwa misingi ya udikteta na pia ni sehemu ya mtandao wa dawa za kulevya nchini kwake.

Kwa upande wake, Umoja wa Afrika (AU) umeibuka na kutoa tamko juu ya kile kilichotokea Venezuela.

AU imekiri kusikitishwa na kile kilichofanywa na Marekani, ikisema kimeingilia mamlaka ya Venezuela, jambo ambalo linakiuka sheria za kimataifa.

Je, ni ipi mtazamo wa wachambuzi wa siasa barani Afrika? Wanaiona hatari ya nchi za Afrika kukutwa na kile kilichotokea kwa Maduro?

Macharia Munene ni mchambuzi na profesa wa Mahusiano ya Kimataifa wa Chuo Kikuu cha Marekani kilichopo mjini Nairobi, Kenya. Anasema:

“Inasikitisha kuona kitendo hicho kimefanywa na nchi inayojinasibu kuwa inalinda sheria za kimataifa.

“Venezuela ni mfano wa kile kinachoweza kuzikuta nchi ndogo pindi zinapokataa kufuata matakwa ya Marekani au mataifa mengine makubwa.”

“Nchi za Afrika ndizo zitakazoingia kwenye shida zaidi. Swali ni je, zitajilinda vipi zisiingie kwenye majaga ya aina hiyo.”

Kwa upande wake, mchambuzi Remi Dodd amesema hofu ya mataifa ya Afrika imesababisha hata yashindwe kulaani hadharani kile kilichoitokea Venezuela.

“Nigeria imekaa kimya, haijalaani hatua hiyo ya Marekani. Ni kama ilivyo kwa Misri, Ethiopia na Kenya. Hata nchi zenye sera za kupinga ubebari kama Namibia, zimekaa kimya.”

Mtaalamu huyo, Dodd, anaamini ukimya wa mataifa ya Afrika unatokana na hofu ya kuharibu uhusiano wao na Marekani.

Aidha, Chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC, kimelaani na kusema kukamatwa kwa Maduro ni wazi Marekani imeamua kukiuka sheria za kimataifa.

Akizungumzia hilo, mchambuzi Macharia Munene anasema utajiri wa rasilimali ya mafuta ni chanzo cha Marekani kuivamia Venezuela, hivyo haitashangaza kuona mataifa ya Afrika nayo yakafuata.

“Afrika nayo ni tajiri wa mali-ghafi. Sasa tunaweza kujiuliza, ni nani anafuta (kushambuliwa na Marekani)?,” amesema.

Kama itakumbukwa, ni miezi michache tu imepita tangu Trump alipoitangazia Nigeria kuwa huenda akaingia kama haitajirekebisha.

Trump anazitaja mamlaka za Nigeria kushindwa kumaliza mauaji dhidi ya Wakiristo, akidai yanafanywa na wenzao wa Dini ya Uislam.

Wakati huo huo, Marekani imekuwa na msuguano mkali na Serikali ya Afrika Kusini kwa madai kuwa haijafanya vya kutosha kudhibiti unyanyasaji dhidi ya watu weupe nchini humo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img