10.2 C
New York

Njama ya kumuua Kapteni Ibrahim Traoré yagonga mwamba

Published:

WAGADUGU, Burkina Faso

SERIKALI ya Burkina Faso imetangaza kuzuiwa kwa njama ya kumuua kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, Kapteni Ibrahim Traoré.

Kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa nchi hiyo, Mahamadou Sana, mpango huo ulipangwa na Luteni Kanali Paul Henri Damiba, aliyekuwa kiongozi wa kijeshi kabla ya kuondolewa madarakani na Traoré Septemba 2022. Taarifa hiyo ilitolewa kupitia hotuba ya usiku wa manane.

Amesema shirika la ujasusi la taifa liligundua na kuzuia njama hiyo katika hatua za mwisho, ikihusisha mpango wa kumuua mkuu wa nchi na kushambulia taasisi nyingine muhimu pamoja na watu mashuhuri. Waziri huyo alidai kuwa njama hiyo iliandaliwa kutoka nchi jirani ya Ivory Coast.

Hadi sasa, hakuna tamko rasmi lililotolewa na Kanali Damiba wala serikali ya Ivory Coast kuhusu tuhuma hizo.

Tangu alipochukua madaraka, Kapteni Traoré amekabiliwa na majaribio mawili ya mapinduzi, huku nchi hiyo ikiendelea kushuhudia ongezeko la mashambulizi ya makundi ya wanajihadi yaliyosababisha mamilioni ya raia kuyahama makazi yao.

Licha ya changamoto hizo, kiongozi huyo wa kijeshi mwenye umri wa miaka 37 ana uungwaji mkono mkubwa ndani na nje ya nchi, hususan kutokana na msimamo wake wa kuhimiza umoja wa Afrika na ukosoaji wake dhidi ya nchi za Magharibi.

Waziri Sana amesema serikali ilifanikiwa kupata video iliyovuja ikionyesha washukiwa wakijadili kwa kina mpango wa kumuua rais kwa njia mbalimbali, ikiwemo shambulio la karibu au kwa kutumia vilipuzi nyumbani kwake mnamo Jumamosi, Januari 3.

Aidha, walipanga pia kuwalenga maafisa wengine waandamizi wa kijeshi na raia. Waziri huyo amedai Damiba alikusanya wanajeshi na raia, akapata ufadhili wa kigeni zaidi ya faranga milioni 70 za CFA kutoka Ivory Coast, na kupanga kuharibu kambi ya ndege zisizo na rubani kabla ya kuingilia kati kwa vikosi vya kigeni.

Amesema watu kadhaa wamekamatwa na uchunguzi unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani, ingawa hakutaja idadi yao.

Kanali Damiba aliiongoza Burkina Faso kuanzia Januari hadi Septemba 2022 baada ya kupindua serikali ya kiraia. Baada ya kuondolewa madarakani, alikimbilia uhamishoni nchini Togo na baadaye kutoa ujumbe mitandaoni akimtumia Traoré salamu za heri.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img