JOHANNESBURG, Afrika Kusini
DJ maarufu wa Afrika Kusini, Warrick Stock, akifahamika zaidi kwa jina ‘DJ Warras’, ameuawa kwa kupigwa risasi mjini Johannesburg.
Polisi wamesema Dj Warras mwenye umri wa miaka 40 alivamiwa na watu watatu, ambapo mmoja wao ndiye aliyemmiminia risasi.
Baada ya kupigwa risasi, staa huyo aliyekuwa mwajiriwa wa moja ya vituo vya redio, alijaribu kukimbia lakini alianguka na kupoteza maisha.
Katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC), dada yake aitwaye Nicole Stock ameeleza kusikitishwa na taarifa za kifo cha Dj Warras.
“Nimeshitushwa. Sina la kusema. Nimechanganyikiwa. Tunajua alikuwa sauti ya watu wengi hapa nchini,” amesema Nicole akiiambia SABC.
Kwa mujibu wa polisi, bado chanzo cha tukio hilo hakijafahamika na hakuna aliyekamatwa, ingawa uchunguzi unaendelea.


