LONDON, Uingereza
BAADA ya kila timu kucheza mechi 11 msimu huu, Manchester City iko kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya England (WSL), ikiizidi pointi sita Chelsea inayoshika nafasi ya pili.
Chelsea, si tu ni mabingwa watetezi, bali pia wamelibeba taji hilo kwa misimu yote sita ya hivi karibuni.
Arsenal inashika nafasi ya tatu, ikifuatiwa na Manchester United na Tottenham zinazoifanya vita ya kuwania ‘Top Four’ kuwa na ushindani mkali. Ni pointi nne pekee zinazotenganisha timu hizo.
Tottenham haikuwa vizuri msimu uliopita kwani ilimaliza katika nafasi ya 11 lakini safari hii ni kama imezaliwa upya chini ya kocha mpya, Martin Ho.
Timu hiyo imeshinda mechi sita kati ya 11 msimu huu wa WSL, ambapo pia ilipata sare katika michezo migumu dhidi ya Arsenal na Man United.
Msimu uliopita (2024-25) haukuwa mzuri kwa Man City kwani waliishia nafasi ya nne kwenye msimamo na kukosa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Safari hii, Man City ni wa moto baada ya ushindi wa mechi 10 kati ya 11 walizoshuka dimbani, hivyo kukusanya pointi 30.
Chelsea wao wamedondosha pointi tisa katika michezo yao 11. Kabla ya kufungwa na Everton mwanzoni mwa mwezi huu, Blues walikuwa wamecheza mechi 34 bila kupoteza.
Kwa upande mwingine, hali ni mbaya kwa vigogo wa mjini Merseyside, Liverpool, tangu msimu huu wa WSL ulipoanza.
Liverpool, ambayo imekusanya pointi mbili pekee katika mechi 11, iko kwenye nafasi za chini kwenye msimamo, kama ilivyo kwa West Ham United.


