LONDON, Uingereza
LICHA ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wolves, Arsenal walilazimika kusubiri hadi dakika ya 66 kupiga shuti lililolenga lango la wapinzani wao hao.
Washika Bunduki hao wa London walipata shuti hilo na kuandika bao kupitia kwa kiungo wake raia wa England, Declan Rice.
Wakati mchezo ukionekana kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Arsenal walipata faida kwa bao la kujifunga la Yerson Mosquera katika dakika ya 94.
Wolves imekuwa timu ya kwanza Ligi Kuu ya England (EPL) kuifanya Arsenal ikiwa nyumbani isipige shuti lililolenga lango kwa muda mrefu wa mchezo tangu Januari, 2019.
Kwa mujibu wa historia, mara ya mwisho kwa Arsenal kubanwa mbavu kiasi hicho ilikuwa katika mchezo wa EPL dhidi ya Cardiff City.


