Na Hassan Mwasha, Gazetini
YANGA haitaonekana uwanjani hadi mwakani. Ikimaanisha, ‘Timu ya Wananchi’ imeshafunga ukurasa wake kwa mwaka 2025. Katika makala haya, Gazetini inakuibulia uchambuzi wa takwimu za Wanajangwani hao kwa mwaka 2025.
Je, unajiuliza Yanga wamemaliza mwaka 2025 wakiwa wamecheza mechi ngapi, matokeo yalikuwaje na wamefunga mabao mangapi? Endelea kusoma.
Kwa ujumla, mabingwa hao wa historia Ligi Kuu Tanzania Bara wameumaliza mwaka huu wa 2025 wakiwa wamecheza jumla ya mechi 36.
Ligi Kuu Bara bila kufungwa
Yanga wamefunga mwaka 2025 wakiwa wameshuka dimbani mara 21. Katika mechi hizo, ‘Timu ya Wananchi’ haijafungwa, na badala yake imeshinda 19 na kutoa sare mbili.
Timu zilizopoteza mbele ya Yanga kwa mwaka huu (kwenye Ligi) ni Kagera, Ken Gold, KMC (2), Singida, Mashujaa, Pamba FC (2), TRA, Coastal (2), Azam, Fountain Gate (2), Namungo, Prisons, Dodoma Jiji, Simba na Mtibwa Sugar.

Timu pekee zilioambulia sare kwa Yanga katika mechi za Ligi Kuu za mwaka huu ni Mbeya City (0-0) na JKT Tanzania (0-0).
Mabao ya Ligi Kuu
Katika mechi zake 21 za Ligi kwa mwaka huu, Yanga imeonekana kuwa moto wa kuotea mbali mbele ya nyavu za wapinzani, ambapo imefunga jumla ya mabao 64.
Wakati huo huo, Yanga ilikuwa bora pia katika eneo la ulinzi kwani iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano pekee katika mechi 21 za Ligi Kuu mwaka 2025.
Vipigo vikubwa zaidi
Kwa mwaka 2025, Yanga imeshuhudiwa ikitembeza ‘dozi’ kubwa mara tano katika mechi zake 21 za Ligi Kuu.
Itakumbukwa kuwa timu zilizokutana na dozi kubwa zaidi mbele ya Yanga ni Ken Gold (6-1), KMC (6-1), Mashujaa (5-0), Prisons (5-0), na Dodoma Jiji (5-0).
Moto wa kimataifa
Kwa mwaka 2025, Yanga imecheza mechi 10 za kimataifa, ikiwamo moja ya kirafiki dhidi ya Rayon Spors ya mjini Kigali, Rwanda. Mechi tisa ni za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi 10 hizo, Yanga imeweza kuibuka na ushindi mara saba, imefungwa moja na kutoa sare mbili. Mabao ya kufunga ni 15, huku ya kufungwa yakiwa ni matatu pekee.
Ushindi wa kimataifa ni dhidi ya TP Mazembe (3-1), Al Hilal (1-0), Rayon (3-1), Wiliete (5-0), Silver Strikers (2-0), na FAR Rabat (1-0).
Mechi pekee waliyofungwa ni dhidi ya Silver (1-0), huku sare mbili zikipatikana katika michezo walizokutana na MC Alger (0-0) na Kabylie (0-0).
FA nako ubabe tu
Mwaka 2025 umekuwa wa mafanikio pia kwa Yanga katika ushiriki wao kwenye michuano ya FA. Katika mechi zao nne, walishinda zote walizokutana na Songea United (2-0), Stand United (8-1), JKT Tanzania (2-0) na Singida United (2-0).

Kwamba wakati wachezaji wa eneo la ushambuliaji wakifanya kazi nzuri ya kufunga jumla ya mabao 14, safu ya ulinzi iliruhusu bao moja pekee.
Wafalme wa ‘Kariakoo derby’
Kwa mwaka 2025, Yanga imepata ushindi katika mechi zote mbili ilizokutana na wapinzani wao wakubwa katika soka la nchi hii, Simba SC.
Mchezo wa kwanza ni ule wa Juni 25, ambapo Yanga wakiwa wenyeji walipata ushindi wa mabao 2-0. Timu hizo zilizopokutana tena Septemba 16 katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Yanga ilishinda bao 1-0.


