Na mwandishi wetu, Gazetini
BAADA ya kuita wachezaji 55 katika kikosi cha awali, kocha wa timu ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’, Miguel Gamondi, amepitisha panga na kubakiza 28 pekee, ambao ndiyo atakaokwendao Morocco.
Stars itashiriki fainali za Mataifa Afrika za mwaka huu (AFCON 2025) zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, mwaka huu.
Katika fainali hizo, Stars iko Kundi C, ambalo pia lina Uganda, Tunisia na Nigeria ‘Super Eagles’.
Kati ya mastaa 27 walikatwa, licha ya kuwa sehemu ya wale 55 walioitwa awali, ni kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya.
Wengine ni mshambuliaji wa Simba, Selemani Mwalimu, Offen Chikola wa Yanga, na staa wa Azam, Nassor Saadun.
Kwa upande mwingine, nahodha wa Stars, Mbwana Samatta, ambaye kwa sasa anakipiga Le Havre ya Ufaransa, ameitwa kikosini kuliongoza safu ya ushambuliaji.
Ni kama ilivyo kwa staa mwenzake wa kikosi, Simon Msuva, ambaye anaitumikia Al Talaba ya Iraq.
Wachezaji 28 walioitwa kikosini ni kama ifuatavyo; Yakoub Suleiman, Hussein Masalanga, Zubeir Foba, Shomari Kapombe, Bakari Mwamnyeto na Lusajo Mwaikenda.
Wengine ni Mohamed Hussein, Nickson Kibabage, Alphonce Mabula, Wilson Nangu, Novatus Dismas na Morice Abraham, Yusuph Kagoma, Kelvin Nashoni na Haji Mnoga.
Pia, kikosi kina Ibrahim Abdullah, Dickson Job, Habibu Iddi, Tarryn Allarakhia, Charles M’mombwa, Pascal Msindo, Feisal Salum, Abdul Suleiman, Idd Selemani, Kibu Denis na Kelvin John.
Kwa mujibu wa ratiba ya fainali hizo, Stars itatupa karata yake ya kwanza Desemba 27 kwa kumenyana na Uganda ‘The Cranes’.


