12.7 C
New York

Kitabu cha Diara kina ukurasa wa Guardiola

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

ACHANA na akina Pacome Zouzoua. Kama kuna jambo linalowapa jeuri mashabiki, viongozi na benchi la ufundi la Yanga, ni uwepo wa Djigui Diara katika lango lao.

Kwa Diara, unapata mambo matatu ndani ya dakika 90 za mchezo mmoja. Uwe wa Ligi Kuu Bara, michuano mwingine ya ndani, au kimataifa, Diara atakupa mambo yote matatu.

Kwanza, atakupa uwezo mkubwa wa kuokoa mabao ya wazi. Kama umesahau hilo, nenda kairudie mechi yao ya kimataifa iliyopita dhidi ya Waarabu wa Algeria, RS Kabylie.

Nilimsikia beki wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, akisema kama si Diara, basi wangepoteza mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Nanukuu: “Nilikuwa namkubali Diara tangu zamani, ila kile alichokifanya (dhidi ya Kabylie) kimenifanya nimuheshimu zaidi.”

Huyo ndiye Diara. Imekuwa ni kawaida yake kuibuka shujaa na kuokoa jahazi katika mazingira ambayo kila mtu angeamini timu imesharuhusu bao.

Pili, Diara ni kiongozi ndani ya uwanja. Kwa umri na uzoefu alionao, amekuwa ni zaidi ya nahodha kwa wachezaji wenzake.

Katika mechi nyingi tu, ameshuhudiwa akiwakaripia wachezaji wenzake, hasa wale wa safu ya ulinzi, lengo likiwa ni kuwakumbusha majukumu yao. Akina Dickson Job wanaweza kuwa mashuhuda wazuri.

Tatu, Diara atakupa uwezo wa kucheza kwa miguu. Ni tofauti na makipa wengi, hasa wa hapa nchini, ambao wamebaki kutekeleza jukumu la msingi (kuzuia mpira usiingie wavuni).

Katika sifa hii ya tatu, hapa ndipo unaoikuta simulizi ya Pep Guardiola na kipa wa zamani wa Manchester City, Joe Hart. Ilikuwaje?

Ni miaka tisa iliyopita. Guardiola aliajiriwa kuinoa Man City na kusaini mkataba wa miaka mitatu. Alipotua, alimkuta Hart akiwa ndiye kipa chaguo la kwanza pale Etihad.

Guardiola akasema haiwezekani. Licha ya kuvutiwa na uwezo wake mkubwa wa kuokoa michomo, Guardiola alionao bado Hart anakosa sifa moja. Uwezo wa kucheza kwa miguu.

Licha ya ushawishi mkubwa alipokuwa nao Hart kwa mashabiki na hata viongozi wa Man City, Guardiola akamtoa kwenye mipango yake. Akamsajili Claudio Bravo kutoka Barcelona.

Huenda Hart alikuwa mzuri zaidi kuliko Bravo katika kuokoa michomo, lakini Guardiola aliamini kipa wa kisasa anahitaji kuwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi kwa kucheza na mabeki wake, kabla ya mpira kuhamia kwenye eneo la kiungo, kisha kuwafikia washambuliaji.

Kwa Guardiola, kipa ndiye anayeuona uwanja kwa ukubwa zaidi. Hivyo, anapocheza na walinzi wake, ni rahisi kwake kuona mianya ya kupitisha mpira kuwafikia viungo au washambuliaji.

Ndicho anachokifanya Diara. Tangu kusajiliwa kwake, licha ya makocha kuingia na kutoka, aina ya uchezaji wa Yanga imebaki kwenye misingi ya Diara, yaani kipa kuwa sehemu ya kuanzisha shambulizi.

Haikushangaza kuona Simba wakimsajili Moussa Camara, ambaye pia ni tofauti na Hart kutokana na uwezo wake wa kucheza kwa miguu.

Huenda usingetarajia kusikia viongozi wa Simba wakikiri, lakini ni wazi uamuzi wa kumfuata kipa aina ya Camara ulitokana na kile walichokiona kwa wapinzani wao, Yanga, kupitia kwa Diara.

Leo hii, Diara, kama ilivyo pia kwa Camara, ni kiigizo (role model) kwa makipa wengi wa Tanzania, ambao sasa wanajaribu kujenga utamaduni wa kucheza kwa miguu na kuanzisha mashambulizi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img