Na mwandishi wetu, Gazetini
JESHI la Polisi Tanzania limesema hali ya usalama nchini ni shwari, huku likitoa onyo kali kwa baadhi ya viongozi wa dini, siasa na wanaharakati wanaodaiwa kuhamasisha vitendo vya uhalifu, vurugu na uharibifu wa miundombinu pamoja na mali za umma na binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumatatu, Oktoba 26, 2026, katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dodoma, Msemaji wa Jeshi hilo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, amesema wamebaini kuwepo kwa mipango na matamko yanayodaiwa kulenga kuwashawishi wananchi kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Misime amesema uhamasishaji huo unafanyika kwa njia mbalimbali, ikiwamo kupitia vikao vya ndani na matamko ya hadharani.
“Kumekuwepo na mipango, matamko na uhamasishaji unaofanywa na baadhi ya viongozi wa dini, siasa na wanaharakati kisirisiri kupitia vikao vya ndani na uhamasishaji wa wazi wenye nia au mwelekeo wa kutaka kuhamasisha watu kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu,” amesema Misime.
Amesema Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, linaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa zinazolihusu suala hilo na kwamba halitasita kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kujihusisha na mipango hiyo.
“Tunaonya wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo vya uhalifu vyenye mwelekeo wa kusababisha fujo na kuharibu mali waache, kwani Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria dhidi ya yeyote atakayebainika kujihusisha na mipango hiyo ya kihalifu,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu, kutii sheria za nchi na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama.
Jeshi hilo limesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi katika kudumisha amani na utulivu nchini.


