18.3 C
New York

Ndejembi aridhishwa na ujenzi wa kituo cha umeme Iganjo

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Iganjo mkoani Mbeya, ambao umefikia asilimia 93 ya utekelezaji.

Ndejembi ameeleza kuridhishwa kwake leo, Oktoba 16, 2026, alipotembelea kituo hicho kinachotekelezwa chini ya Mradi wa Tanzania–Zambia Transmission Interconnector (TAZA), unaolenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme na kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa, pamoja na kuchochea shughuli za uchimbaji madini, ukuaji wa viwanda, uwekezaji na kuongeza fursa za ajira, hususan kwa vijana.

“Umeme utakaofika hapa si kwa ajili ya nchi jirani ya Zambia pekee, bali pia utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa. Naipongeza sana Wizara ya Nishati kupitia Tanesco kwa kazi nzuri iliyofanyika. Nilipofika hapa mwezi Machi, mradi ulikuwa katika hatua za awali, lakini kwa sasa uko mbioni kukamilika. Kwa maendeleo haya, nimeridhika na nilichokiona,” amesema Mhe. Ndejembi.

Ameongeza kuwa kituo hicho kitakuwa na mchango muhimu katika kuboresha upatikanaji wa umeme kwa shughuli za kiuchumi na kuwezesha usafirishaji wa umeme kwenda nchi jirani, ikiwemo Zambia.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya nishati unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme na kufungua fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ameeleza kuwa Kituo cha Iganjo kitakuwa na uwezo wa kusambaza umeme katika maeneo yenye mahitaji makubwa, ikiwemo Saza mkoani Songwe, ambako shughuli za uchimbaji madini zinahitaji umeme wa uhakika, pamoja na kuwezesha usafirishaji wa umeme kwenda nchi jirani ya Malawi.

“Kazi hii inafanyika kwa kasi kubwa kutokana na umuhimu wake katika maendeleo na kufungua fursa za kijamii na kiuchumi. Kituo hiki cha Iganjo pia kitakuwa na uwezo wa kupeleka umeme katika eneo la Saza mkoani Songwe, ambako kuna uhitaji mkubwa wa umeme kwa shughuli za uchimbaji madini, pamoja na nchi jirani ya Malawi,” amesema Mhe. Makamba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema ujenzi wa Kituo cha Iganjo unagharimu takribani shilingi bilioni 175 na umefikia asilimia 93 ya utekelezaji.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na maeneo jirani, yakiwemo Uyole, Mbarali, Tukuyu na Busokelo, kupitia miundombinu ya kusafirisha umeme.

“Mradi huu una umuhimu mkubwa katika kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Uyole, Mbarali, Tukuyu na Busokelo, kupitia ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme,” amesema Twange.

Aidha, Twange amesema ifikapo Desemba 5, 2026, Kituo cha Iganjo kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kupokea umeme unaozalishwa katika Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), kufuatia kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Zuzu mkoani Dodoma hadi Tagamenda mkoani Iringa.

Mradi wa TAZA unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga mkoani Rukwa na unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi trilioni mbili.

Mradi huo unalenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme, kuongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo na kuwezesha biashara ya umeme kati ya Tanzania na nchi jirani, hatua inayotarajiwa kufungua fursa zaidi za uwekezaji na kukuza shughuli za kiuchumi katika maeneo yatakayohudumiwa na miundombinu hiyo.

Related articles

Recent articles