LOS ANGELES, Marekani
UTATA uliodumu wa miaka 30 umepatiwa ufumbuzi hivi karibuni baada ya Duane Davis, maarufu kwa jina la Keffe D, kukutwa na hatia katika kesi ya mauaji ya rapa Tupac Shakur.
Kwamba Keffe D ndiye aliyemuua kwa kumpiga risasi Tupac katika tukio la mwaka 1996 mjini Las Vegas, wakati huo rapa huyo akiwa na mafanikio makubwa kwenye muziki wa Hip hop, licha ya umri wake mdogo wa miaka 25.
KEEFE D ALIVYOJIKAANGA
Ushahidi wa Keefe D kumuua Tupac ulitokana na kauli zake mwenyewe kupitia makala, filamu yake fupi, vipindi vya televisheni yake ya mtandaoni, na mahojiano yake na polisi.
Wakati huo akiwa hajafunguliwa mashitaka, alikiri kuhusika katika kifo cha Tupac, akisema ndiye aliyefyatua risasi kumlenga staa huyo katika tukio la Septemba 7, 1996.
Kwamba licha ya kutokuwepo kwa shuhuda wa tukio, kauli zake ndizo zilizotumika kama ushahidi mbele ya mahakama, ingawa wanasheria wake wamesema hilo halikubaliki na watakata rufaa.
Kwa mujibu wao, mahakama imemkuta na hatia ikiwa haina shuhuda, silaha iliyotumka wala video au picha za siku ya tukio, wakisisitiza kuwa kulikosekana hata ushahidi kuthibitisha kuwa Keefe D alikuwa Las Vegas siku hiyo ya tukio.
Yote kwa yote, mahakama inaamini kuwa Keefe D amehukumiwa kwa kauli zake na huenda asingefunguliwa mashitaka endapo angeamua kukaa kimya (kuhusu kifo cha Tupac).
NI ZAMU YA B.I.G.?
Sasa, baada ya aliyemuua Tupac kufahamika, inaibua picha kwamba huenda sasa dunia ina hamu ya kumjua aliyemuua aliyekuwa mpinzani wake mkubwa kimuziki, Christopher Wallace ‘Notorious B.I.G.’.
B.I.G. naye aliuawa miezi sita tu baada ya kifo cha Tupac, tena kwa staili ile ile ya Tupac. Aliminiwa risasi Machi 9, 1997, wakati anatoka katika ‘party’ ya Tuzo za Soul Train Music mjini Los Angeles.
Kama ilivyokuwa kwa Tupac, tukio lilitokea kwenye foleni, ambapo B.I.G. akiwa kwenye gari, ghafla watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari aina ya Chevrolet walianza kummiminia risasi.
Kutokana na uhasimu wao wa kimuziki wakati huo, wengi wanaona pande mbili hizo zilidhuriana. Kwamba B.I.G. alihusika kifo cha Tupac, na watu wa mwenzake huyo wakalipiza kisasi.
Ni kutokana na hilo, mwandishi maarufu wa habari za muziki, Justin Tinsley, anaamini hakuna namna unayoweza kutofautisha uhusiano unaoweza kuwepo kati ya kifo cha Tupac na kile cha B.I.G.
“… Ni ngumu kueleza stori ya upande mmoja, bila kugusa mwingine. Unapozungumzia kesi hizi, mara zote zimeonekana kuhusiana kwa sababu wapo baadhi ya watu wanaotajwa (kuhusika) katika pande zote,” amesema Tinsley.
Miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakitajwa pande zote mbili ni Keffe D, ikielezwa kuwa alifahamiana vizuri na B.I.G, na alikuwapo kwenye ‘party’ siku ambayo rapa huyo aliuawa.


