Na mwandishi wetu, Gazetini
KAMA tulivyoanza katika sehemu iliyopita, mauaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 yaliwahusisha Wahutu na Watutsi, ambayo ndiyo makabila makubwa zaidi nchini humo.
Kabila la tatu kwa ukubwa ni Twa lakini linachangia asilimia moja tu ya raia wa Taifa hilo dogo zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa pamoja, mataifa yote matatu yanazungumza Kinyarwanda.
Kwa mujibu wa historia, eneo linalofahamika kama Rwanda kwa sasa lilianza kukaliwa na watu wa jamii ya Twa, kabla ya Wahutu nao kuingia kati ya karne ya 5 hadi 11. Watusti walianza kuingia katika karne ya 14.
Hata hivyo, hadi Wazungu wanaingia Rwanda katika karne ya 19, jamii ya Watutsi ndiyo iliyokuwa ikitawala eneo hilo, sasa likifahamika kwa jina la Rwanda.
Tofauti na Watutsi waliojikita zaidi katika shughuli za ufugaji, Wahutu wao walijishughulisha na kilimo. Pia, mionekano yao ilitofautiana; Watutsi walikuwa weupe na warefu, wakati Wahutu walikuwa weusi na wafupi.
Hata hivyo, katika maisha ya kila siku, haikuwa rahisi kuziona tofauti zao kwani mwingiliano wa kuoleana na kutumia lugha moja ulikuwa mkubwa miongoni mwa watu wa jamii mbili hizo.
Changamoto ilikuja wakati wa ukoloni. Wajerumani walioiongoza Rwanda kuanzia mwaka 1898, kisha Wabelgiji walioichukua nchi baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia.
Kwa pamoja, licha ya kwamba ni kwa nyakati tofauti, wazungu walianza kuzigawa jamii hizo, ambapo waliwatumia Watutsi kuitawala Rwanda, wakiwapa nafasi za chini za uongozi.
Hali hiyo haikuwafurahisha Wahutu na taratibu ikaanza kutengeneza mpasuko, kujenga chuki, na kuondosha umoja na mshikamano katika jamii. Wahutu wakaamka na kuanza kudai usawa, wakisaidiwa na Kanisa Katoliki na baadhi ya viongozi wa serikali ya kikoloni.
Mapinduzi ya Wahutu yakafuata Novemba 1, 1959, baada ya tetesi zilizodai kuwa kiongozi wa wao ameuawa akiwa mikononi mwa Watutsi. Wahutu wakaanza kuwashambulia watu wa jamii ya Watutsi.
Miezi kadhaa ya machafuko hayo yalishuhudia Watutsi wengi wakiuawa na wengine kulazimika kuikimbia nchi. Hatimaye, Wahutu waliweza kumng’oa mfalme wa Watutsi mwaka 1961.
Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika, kuanzia mwaka 1959 hadi 1961, Watutsi zaidi ya 20,000 waliuawa na wengi walilazimika kukimbilia nchi jirani ili kuyanusuru maisha yao.
Hivyo basi, hadi Rwanda inapata uhuru wake mwaka 1962, Wahutu ndiyo waliokuwa wanatawala zaidi, wakiongoza kwa idadi kubwa kwenye nafasi za uongozi.
Kufikia mwanzoni mwa mwaka 1964, Watutsi takribani 150,000 walikuwa wakiishi nchi jirani wakihofia kurudi Rwanda. Pia, yaliripotiwa mauaji dhidi yao katika miaka ya 1963, 1967 na 1973.
Usikose sehemu ya tatu ya makala haya. Tembelea www.gazetini.co.tz.


