22.9 C
New York

Uratibu wa maafa sasa kidijitali zaidi, Serikali yawaita wadau

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

AGOSTI 19 ya kila mwaka, Tanzania, kama zilivyo nchi zingine duniani, huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Misaada ya Kibinadamu. Kwa kuyataja maafa hayo kwa uchache, ni pamoja na magonjwa ya mlipuko, moto na mafuriko.

Katika kuiendea Siku hiyo kwa mwaka huu, juzi Agosti 18, 2026 lililafanyika Kongamano katika Ukumbi wa Danken jijini Dar es Salaam, likiratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kupitia Idara yake ya Menejimenti ya Maafa, mgeni rasmi akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, James Kilabuko.

Mbali na Serikali, Kongamano hilo liliwaleta pamoja wadau mbalimbali wa maafa (asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa, na waandishi wa habari) kujadili miundo ya utekelezaji wa misaada ya kibinadamu, dharura ya afya ya jamii na dhana ya ‘Afya Moja’ (One Health), na mchango wa teknolojia katika udhibiti wa maafa.

MIUNDO YA URATIBU WA MISAADA YA KIBINADAMU

Kwa nafasi yake, Mratibu wa masuala ya Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Winfrida Ngowi, alieleza kwa kina historia na muundo wa uratibu wa maafa hapa nchini.

Alisema kabla ya mwaka 1990, hakukuwa na uratibu wa pamoja kama ilivyo sasa chini ya Idara, na badala yake kila taasisi ilifanya kwa upande wake, hivyo kusababisha kukosa ufanisi, gharama kubwa kutumika, na hata kujirudia kwa misaada katika eneo moja la maafa.

“Mwaka 1990, ndipo ikatungwa sheria iliyoasisi Idara ya Menejimenti ya Maafa, kisha ukaanzishwa Mfuko wa Taifa wa Maafa. Mwaka 2022, katika kuboresha zaidi, ilitungwa sheria mpya.

“Idara inaongozwa na Mkurugenzi, pia ikiwa kwenye ngazi zote, kuanzia Taifa, Mkoa, Wilaya na pia tunazo Kamati za Kata,” alisema bi. Winfrida.

Je, ni yapi majukumu ya Idara hiyo? Akieleza zaidi, alisema Idara imekuwa ikifanya tathimini na tafiti za kabla, wakati na baada ya maafa, achilia mbali kutoa elimu ya kujikinga, pamoja na kutafuta rasilimali.

“Kabla ni kwa maana ya kujiandaa na maafa yanayoweza kutokea. Na yanapotokea, tunafanya tathmini ya kina na kutoa huduma. Baada ya maafa, bado tuna wajibu wa kufuatilia (kwa muda mrefu au mfupi) hali ya waathirika au maeneo yaliyopata maafa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Kanali Selestine Masalando, alisema licha ya maboresho yaliyofanyika, ikiwamo Sera mpya ya Maafa ya mwaka 2025, zipo changamoto zinazoikumba Idara hiyo ya Menejimenti ya Maafa.

“Kwanza, ni ukosefu wa fedha za kutosha. Hili ni tatizo la dunia nzima. Lazima tuwe na fedha za kutosha ili kutekeleza miongozo iliyopo. Pili, elimu inahitaji ili kujenga uwezo si tu kwa wafanyakazi, bali pia kwa wananchi,” alisema Kanali Masalando.

Hata hivyo, alisema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya jitihada kubwa na sasa upo Mfuko wa Mafaa katika Wizara ya Fedha, pia akisisitiza kuwa bado upatikanaji wa taarifa na tofauti ya uzoefu kati ya eneo moja na jingine ni changamoto zingine.

“Katika eneo ambalo lilishawahi kupata maafa, walau unakuwepo uelewa wa namna ya kukabiliana nayo, tofauti na eneo ambalo linapata maafa kwa mara ya kwanza,” alisema.

Wakati huo huo, si tu Serikali Kuu, bali pia Idara imekuwa ikishirikiana kwa karibu na asasi za kiraia na mashirika ya nje ya nchi katika uratibu wa maafa kila yanapojitokeza.

CAN Tanzania ni Mtandao wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na ni moja ya wadau walioshiriki Kongamano hilo. Kupitia mwakilishi wake, Prince Batamuzi, ambaye ni Mtaalamu wa Misitu na Taarifa za Kijiografia, CAN ilieleza mchango ilionao katika kukabiliana na maafa.

“Tumejikita katika halimashauri na Serikali za Mitaa, tukiamini ndizo zilizo karibu zaidi na maafa pindi yanapotokea. Hata hivyo, changamoto kubwa tunayoiona ni halimashauri kukosa fedha zilizotengwa kwa ajili ya maafa. Vipaumbele ni vingi.

“Pia, wataalamu waliopo katika baadhi ya maeneo hawana uwezo wa kutosha. Sambamba na hilo, bado hakuna ‘coordination’ (uratibu). Unakuta NGO’s (asasi za kiraia) ziko eneo moja lakini kila moja inafanya kazi kivyake katika kukabilana na maafa, ” alisema Batamuzi.

Changamoto hiyo ya kukosekana kwa mpango wa pamoja miongoni mwa NGO’s na mashirika iliibuliwa pia na wadau wengine, wakiwamo Save The Children, DINGONET (Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na Maafa), REDCROSS (Shirika la Msalaba Mwekundu), ambalo pia linafanya kazi katika ngazi zote (Taifa, Mkoa, Wilaya na Kata).

‘AFYA UMOJA’ KATIKA KUDHIBITI MAAFA

‘Afya Umoja’ (One Health) ni dhana inayofanya kazi chini ya Sheria Namba 6 ya mwaka 2022. Ni dhana inayoziweka pamoja sekta za afya ya wanyama, binadamu na mazingira kwa lengo la kushirikishana tafiti na mikakati ya kukabiliana na maafa ya magonjwa.

Kwanini unahitajika ushirikiano wa tafiti? Dkt. Simon Chacha, ambaye ni mtaalamu wa Afya ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, alisema asilimia zaidi ya 65 ya magonjwa ya binadamu hutokana na wanyama pori. Ebola ni mfano mzuri.

Akisisitiza umuhimu wa sekta hizo kusomana ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko, Dkt. Chacha alisema: “Muingiliano (wa binadamu na wanyama) ni mkubwa, hivyo tunahitaji tafiti za kutusaidia kupata ufumbuzi wa pamoja.

“Tatizo ni kwamba unakuta watu wa wanyamapori wanafanya tafiti zao, kisha wanabaki nazo. Sekta ya afya ya binadamu nao wanafanya tafiti na kubaki nazo. Hivyo hivyo kwa upande wa wenzetu wa mazingira. Ni vyema tafiti hizi zikutane ili kupata suluhisho la pamoja.”

Akiongeza katika hilo, mtafiti kutoka Taasisi ya Tafiti za Wanyamapori nchini (TAWIRI), Dkt. Mikidadi Mtalika, alisema: “Kila sekta (ya afya ya wanyamapori, binadamu na mazingira) inafanya tafiti zake. Naamini zitakuwa na mafanikio makubwa katika uratibu wa maafa, hasa magonjwa ya mlipuko, endapo zitashirikishana tafiti.

“Turuhusu hii mifumo iwe inasomana. Kama asilimia kubwa ya magonjwa ya binadamu yanatokana na wanyama, hakuna haja ya kuwepo uzio kati ya tafiti za sekta hizo. Naona tuwe na uwanja mmoja, ambao unaweza kuleta matokeo mazuri katika udhibiti wa maafa, hususani magonjwa ya mlipuko.”

Aidha, eneo jingine lililotajwa kuwa ni changamoto ni jamii kukosa mrejesho baada ya tafiti kufanyika. Akichangia, Dkt. Mikidadi alisema: “Tunakwenda kwenye jamii, tunafanya tafiti, halafu tunaondoka, jamii haipewi majibu.

“Kama wananchi hawapewi majibu na kubadilika, utafiti huo hauna maana. Ni maoni yangu; kama inawezekana, mtafiti alazimishwe kurudi kwenye jamii na kuipa majibu ya utafiti wake.”

TEKNOLOJIA KUKABILIANA NA MAAFA

Akizungumza wakati wa Kongamano hilo, Dkt. Adam Philipo, mtaalamu wa Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Kidijitali kutoka Taasi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), alisema moja ya hatua walizopiga ni matumizi ya ‘drone’ (ndege zisizo na rubani) kupiga picha katika maeneo yenye maafa.

Kwa upande wake, Benjamin Mkwala, ambaye ni Mlinzi wa Taarifa za TEHAMA kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), alisema Taasisi hiyo nayo imekuwa ikitumia teknolojia kwa kiwango kikubwa katika kupata taarifa zake.

“Tumefunga vifaa vya mawasiliano hata kwenye maeneo ambayo hayafikiki na binadamu. Mfano, kwenye Mlima Kilimanjaro na mbuga za wanyama,” alieleza na kuongeza kuwa TMA imekuwa ikitumia pia njia zingine za kijitali, ikiwamo mitandao ya kijamii.

Naye Ofisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambaye pia ni Mhandishi wa Mifumo ya Kompyuta wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TRCA), Gevis Mtweve, alieleza namna wanavyotumia teknolojia kukabilia na maafa.

Alisema: “Tumekuwa tukitumia vyombo vya habari vikuu, kwa maana ya redio na televisheni, na pia meseji za kawaida kwa njia ya simu za mkononi, pamoja na mitandao ya kijamii, lengo likiwa ni kuhakikisha za taarifa za tahadhari juu ya maafa zinawafikia wananchi kwa wakati,” alisema.

Naye Mratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhandisi Abubakar Amanzi, aliongeza kuwa tayari wameanzisha mfumo wa kupata taarifa za maafa kidijitali ili kuboresha ufanisi wake. “Ndiyo, ni mfumo wa ‘e-TAARIFA’, ambao upo katika hatua za ujenzi na kazi yake ni kuratibu taarifa za maafa,” alisema.

Katika mfumo huo, mwananchi anaweza kupata taarifa za maafa mbalimbali, namna ya kujikinga, na pia mawasiliano ya mamlaka husika, mathalan namba ya simu ya kikosi cha zimamoto.

SERIKALI YAFUNGUA MILANGO

Katika hotuba yake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kilabuko, alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wadau katika kuboresha udhibiti wa maafa.

“Sisi kama Serikali, tunaahidi kuendelea kushirikiana na wadau. Ukweli ni kwamba sisi peke yetu hatuwezi ila kwa pamoja tutaweza. Milango yetu iko wazi,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine, alisema mikakati ya kuzuia maafa inapaswa kuwa kipaumbele, badala ya kusubiri yatokee ndipo hatua zichukuliwe. “Hatupaswi kusubiri hadi yatokee. Na yanapotokea, basi misaada iwafike walengwa kwa wakati,” alisema.

Wakati huo huo, Mratibu wa masuala ya Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), bi. Winfrida, alisema wadau wana nafasi muhimu katika utekelezaji wa miongozo ya uratibu wa misaada ya kibinadamu.

“Nawapongeza wadau kwa ushirikiano wao mkubwa. Tumekuwa tukishirikiana vizuri na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali ilimradi kuhakikisha tunaihudumia jamii,” alieleza.

Related articles

Recent articles