Na mwandishi wetu, Gazetini
UDHIBITI wa tatizo la dawa za kulevya hufuata Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015 na miongozo ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).
Aidha, kuna mikakati mikuu minne inayoongoza jitihada za mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
KUDHIBITI UPATIKANAJI (SUPPLY REDUCTION)
Lengo la mkakati huu ni kudhibiti uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini. Upatikanaji wa dawa za kulevya unahusisha kilimo, utengenezaji, uingizaji na usambazaji kupitia mipaka ya nchi kavu, majini na anga.
Utekelezaji wa mkakati huu unahusisha njia juu nne, ambazo ni pamoja na ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa kuhusu biashara ya dawa za kulevya.
Sambamba na hilo, ni ukamataji wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya, usimamiaji wa sheria ya dawa za kulevya nchini, na udhibiti wa uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Mathalan, kwa mwaka 2025, kiasi cha tani 1,014.06 za bangi zilikamatwa zikihusisha watuhumiwa 7,715, kati ya hao wanaume 7,014 na wanawake 701.
Katika kipindi hicho cha mwaka 2025, jumla ya tani 36.18 za dawa za kulevya ziliteketezwa. Mchanganuo wa dawa zilizoteketezwa ni tani 22.06 za bangi, mirungi tani 10.41, tani 2.65 za methamphetamine, tani 1.06 za heroin na gramu 326.95 za cocaine.
KUPUNGUZA UHITAJI (DEMAND REDCUTION)
Mkakati huu umejikita katika utoaji wa elimu ili kuifanya jamii kujitambua na kujiepusha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini.
Katika utekelezaji wa mkakati huu, Mamlaka inaratibu uelimishaji juu ya tatizo la dawa za kulevya katika jamii, ikiwa ni pamoja na kuandaa miongozo ya uelimishaji, kuwaandaa na kuwawezesha watoa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya.
Pia, ni kwa kuratibu asasi zinazotoa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa jamii, kuratibu uanzishwaji na uendeshaji wa klabu za dawa za kulevya na kuhuisha maudhui ya dawa za kulevya kwenye mitaala ya elimu.
KUPUNGUZA MADHARA YA MATUMIZI (HARM REDCUTION)
Lengo la mkakati huu ni kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya. Katika mkakati huu Mamlaka inaratibu huduma za matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya.
Mamlaka inaratibu huduma maalumu za kugawa mabomba kwa waraibu wanaojidunga kuzuia maambukizi ya magonjwa yanayoambukiza kwa njia ya damu (Needle and Syringe Program-NSP), maandalizi ya miongozo ya matibabu.
Pia, ni kwa kuwezesha usimamizi shirikishi katika vituo vinavyotoa huduma za tiba na unasihi pamoja na na utoaji elimu ya kupunguza madhara kwa waraibu.
KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KITAIFA, KIKANDA NA KIMATAIFA
Tatizo la dawa za kulevya ni suala mtambuka linalohusisha mitandao ya kihalifu iliyopo nchi mbalimbali duniani, hivyo mapambano dhidi ya tatizo hili yanahitaji ushirikiano na nguvu za pamoja kuanzia ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Katika utekelezaji wa mkakati huu masuala yafuatayo huzingatiwa; Utekelezaji wa mikataba na miongozo ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika udhibiti wa dawa za kulevya; Ubadilishanaji wa taarifa za kiintelejensia na uzoefu baina ya mataifa kuhusu udhibiti wa dawa za kulevya na kushiriki mafunzo ya pamoja.


