27.2 C
New York

Vichocheo vya kufikia malengo ya Dira 2050: Nishati

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

UPATIKANAJI wa nishati ya uhakika ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii. Umuhimu wa nishati unajidhihirisha kuanzia matumizi ya kila siku majumbani na ofisini hadi katika sekta za viwandani na mifumo ya usafirishaji.

Wakati huo huo, nishati ina mchango mkubwa katika kuboresha viwango vya maisha na kuinua ustawi wa jamii, na hivyo kuleta maendeleo endelevu kwa Taifa.

Tafiti zinaonesha kuwa umeme ni ni nyenzo muhimu katika kuwatoa watu katika umasikini, sambamba na elimu na kiwango stahimilivu cha ongezeko la idadi ya watu.

HATUA ZILIZOPIGWA

Matumizi ya nishati ya umeme kwa kila mtu yameongezeka kufikia wastani wa 170 kWh na yanatarajiwa kuongezeka na kufikia 3,000 kWh ifikapo mwaka 2050.

Baadhi ya jitihada zinazoendelea katika kuimarisha sekta ya nishati ni uwekezaji mkubwa unaolenga kupanua uwezo wa kuzalisha nishati endelevu na ya kuaminika, ikiwamo nishati ya maji, jua, upepo, nyuklia, na jotoardhi.

Mfano halisi wa juhudi hizi ni mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.

Wakati huo huo, juhudi zinaendelea kupunguza upotevu wa nishati wakati wa usambazaji kutoka asilimia 16 hadi chini ya asilimia 10. Ni kwa kuboresha miundombinu ya usambazaji ili kuhakikisha mfumo wa usafirishaji wa nishati unakuwa imara na wenye ufanisi zaidi.

CHANGAMOTO ZILIZOPO

Licha ya maendeleo hayo, bado sekta ya nishati inakabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwamo za miundombinu isiyokidhi mahitaji, usimamizi usioridhisha wa sheria za nishati, na upungufu wa rasilimali fedha.

Kukabiliana na changamoto hizo, kunahitajika juhudi za pamoja ili kuhakikisha uthabiti wa sera, kujenga uwezo wa kiufundi na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

MATARAJIO

Kufikia mwaka 2050, matarajio ni kuiona Tanzania ikiwa na mfumo bora wa nishati safi ulio stahimilivu, wenye ufanisi, wa kuaminika, n awa gharama nafuu.

Pili, kuwa na miundombinu thabiti ya nishati inayochochea maendeleo ya viwanda na ustawi wa kiuchumi ba jamii.

Tatu, ni kuiona Tanzania ikiwa Taifa linalozalisha nishati ya kutosha kukidhi mahitaji ya ndani, huku ikijipambanua kuwa moja ya wazalishaji wakuu wa nishati katika Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Related articles

Recent articles