27.2 C
New York

Bashar al-Assad: Rais ‘dikteta’ aliyeangukia hukumu ya kifo (4)

Published:

DAMASCUS, Syria

WAKATI hali ya utulivu ikiwa haijatengamaa, Syria iliingia katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2021 na Assad kushinda kwa muhula wake wa nne madarakani. Ni Uchaguzi uliompa ushindi wa asilimia 95 ya kura.

Hata hivyo, kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita, wapinzani na hata jumuhiya za kimataifa waliyakataa matokeo, wakisema Uchaguzi haukuwa huru na wa haki, bali Assad aliwekewa mazingira ya kurudi Ikulu.

Nje ya ushindi wake kupingwa, moja ya changamoto zilizomkabili Assad ni hali mbaya ya kiuchumi kwa raia wa Syria. Tayari yalikuwepo malalamiko ya muda mrefu juu ya ugumu wa maisha uliotokana na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu, hasa vyakula.

Hali hiyo ilizaa maandamano makubwa na kwa mara ya kwanza, yalianzia katika maeneo ambayo yalikuwa yakidhibitiwa na wapiganaji wa Serikali. Moja ya hayo ni Jimbo la Suweida.

Katika utetezi wake, Serikali ilidai kuwa hali mbaya ya kiuchumi ilisababishwa na vikwazo ilivyowekewa na mataifa ya Magharibi. Wananchi wakifahamu hilo lakini hawakutaka kuelewa.

Kwanini? Walisikia mara kadhaa shutuma za rushwa serikalini. Pia, familia ya Assad na viongozi wenzake walikuwa na utajiri mkubwa, wengine wakihusishwa kusaini mikataba mibaya na kampuni za nje.

Safari hii, Syria ya Assad ilipaswa kujipambania yenyewe (bila msaada wa Hezbollah wala Urusi) katika maandamano makubwa ya raia waliochoshwa na utawala wake waliamini umekosa suluhisho la changamoto zao.

Hezbollah hawakuweza tena kuingia kwa miguu miwili Syria kwani nao wakati huo walikuwa bize kujibu mashambulizi ya Israel nchini kwao, Lebanon. Urusi nayo ilishaingia kwenye vita na Ukraine.

Bila nguvu ya Hezbollah na Urusi, utawala wa Assad ukaanza kuanguka taratibu, huku wapiganaji wa upinzani waliokuwa wakiungwa mkono na raia wakizidi kuteka miji iliyokuwa ikidhibitiwa na Serikali.

Saa chache tu baada ya taarifa za waasi kukaribia kuingia Mji Mkuu, Damascus, Assad akatangaza kujiuzulu, kisha kukimbilia Moscow, Urusi, akiwa na familia yake.

Hatua hiyo ilipokelewa kwa shangwe na raia wa Syria walioingia barabarani kusherehekea anguko la Assad na huo ukawa mwisho wa safari yake katika kiti cha urais wa Syria.

NB: Hii ni sehemu ya nne na ya mwisho ya makala haya. Kama ulipitwa na sehemu zilizopita, tembelea www.gazetini.co.tz.

Related articles

Recent articles