DAMASCUS, Syria
KAMA ilivyoelezwa katika sehemu ya kwanza ya makala haya, Assad hakutarajiwa kuwa kiongozi wa Syria. Hakuonekana kupenda siasa na kufuata nyayo za baba yake, Hafez al-Assad.
Tuanzie hapa; Assad alizaliwa Septemba 11,1965 akiwa mtoto wa pili wa kiume baada ya kaka yake aitwaye Basil.
Alihitimu elimu ya juu ya masomo ya Afya katika Chuo Kikuu cha Damascus mwaka 1988. Miaka minne baadaye, alitimika London, Uingereza, kwa ajili ya kujiendeleza zaidi.
Hata hivyo, Basil aliyeonekana kuwa mrithi wa baba alifariki kwa ajali ya gari mwaka 1994, hivyo Assad akarejeshwa Syria ili kuandaliwa kwa ajili ya kiti cha urais.
Aliporudi Syria, Assad aliingia katika Chuo cha Jeshi mjini Homs, ambapo alipanda vyeo na hatimaye kuwa kanali mwaka1999 na Katibu Mkuu wa Chama chake cha Baath.
Baba yake alipofariki Juni, 2000, baada ya kuiongoza Syria kwa miaka zaidi ya 20, Assad aliingia Ikulu akiungwa mkono na jeshi, Chama tawala cha Baath, na jamii yake ya Alawite.
Baada ya kuingia madarakani, Assad aliahidi mengi, ikiwamo kukuza uchumi na kuufanya kuwa wa kisasa zaidi, kudhibiti rushwa na kukuza demokrasia nchini humo.
Moja ya hatua zake zilizopongezwa wakati huo ni kuwatoa magerezani mamia ya wafungwa wa kisiasa.
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka zaidi ya 30, Syria ikawa na magazeti ya watu binafsi na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Hata hivyo, mambo yalibadilika ghafla mwanzoni mwa mwaka 2001. Mikutano ikaanza kuzuiwa, huku vyombo vya dola vikiwakamata baadhi ya wanasiasa maarufu wa upinzani.
Mei, 2007, Assad alishinda tena kiti cha urais. Alipata asilimia 97 ya kura, ingawa wakosoaji walilalamikia Serikali kukiuka kwa kiasi kikubwa taratibu za Uchaguzi.
Je, katika eneo la sera za kimataifa, ni upi uliokuwa msimamo wa Syria ya Assad juu ya mgogoro wa Gaza?
Usikose sehemu ya tatu ya makala haya … Tembelea www.gazetini.co.tz


