27.5 C
New York

Benki ya Dunia, Serikali kukamilisha mpango wa kuongeza ajira kwa vijana

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

SERIKALI ya Tanzania na Benki ya Dunia zimefanya kikao cha pamoja cha kuhitimisha maandalizi ya kitaalamu ya Programu ya Uendelezaji wa Ushoroba wa Kati wa Maendeleo ya Kiuchumi Utakaoongeza Ajira kwa Vijana (KAZI MPA), inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini.

Kikao hicho kiliongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais–Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk

. Tausi Kida, kwa upande wa Serikali, na kilifanyika katika Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, kikao hicho kililenga kuwasilisha na kujadili matokeo ya maandalizi yaliyofanywa kwa pamoja kati ya Serikali na Benki ya Dunia, pamoja na kukubaliana hatua zinazofuata kuelekea kukamilisha maandalizi ya programu hiyo.

Katika kikao hicho, pande hizo zilijadili maeneo muhimu ya utekelezaji wa KAZI MPA, huku zikisisitiza umuhimu wa programu hiyo katika kuchochea mageuzi ya kiuchumi, kuongeza uwekezaji na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Programu hiyo, inayotekelezwa kupitia Ushoroba wa Kati, inalenga kuongeza fursa za ajira, hususan kwa vijana, pamoja na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Aidha, KAZI MPA inalenga kuendeleza miundombinu na kuweka mazingira wezeshi kwa shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayohusishwa na Ushoroba wa Kati, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa biashara, uwekezaji na uzalishaji.

Ushoroba wa Kati ni miongoni mwa maeneo yenye umuhimu mkubwa katika kukuza biashara na usafirishaji wa bidhaa, hivyo utekelezaji wa programu hiyo unatarajiwa kuongeza fursa kwa sekta binafsi na wananchi wanaojihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Serikali imeeleza kuwa utekelezaji wa KAZI MPA unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya jitihada za kutafsiri kwa vitendo malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, hususan katika kujenga uchumi wenye tija, jumuishi na stahimilivu.

Kupitia programu hiyo, Serikali inalenga kuweka mazingira yatakayowawezesha wananchi, hasa vijana, kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, biashara na uwekezaji, sambamba na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi.

Kikao hicho ni sehemu ya hatua za mwisho za maandalizi ya kitaalamu ya KAZI MPA kabla ya kuendelea na hatua zinazofuata za utekelezaji wa programu hiyo.

Related articles

Recent articles