30.9 C
New York

Ndejembi awasha umeme Mwanubi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amewasha umeme katika Kitongoji cha Mwanubi mkoani Shinyanga na kusema kuwa huduma ya umeme ni hitaji la msingi kwa Watanzania na nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza leo Jumatatu, Agosti 10, 2026 wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika kitongoji hicho, Ndejembi amesema kufikishwa kwa umeme vijijini kunapaswa kwenda sambamba na matumizi yenye tija, ikiwemo kuongeza thamani ya mazao, kuendeleza biashara na shughuli za uzalishaji pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii.

Amesema Serikali inaendelea kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma ya umeme, hususan katika maeneo ya vijijini, ili nishati hiyo iwe kichocheo cha uzalishaji, ongezeko la kipato na uboreshaji wa maisha ya wananchi.

Ndejembi amewahimiza wananchi ambao miundombinu ya umeme imewafikia kuchangamkia fursa hiyo kwa kuunganishiwa huduma kwa gharama nafuu ya sh 27,000, na kutumia umeme katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na kujiletea maendeleo.

Aidha, ameiagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufanya tathmini ya maeneo ambayo bado hayajafikiwa na miundombinu ya umeme ili yaingizwe katika mipango ya utekelezaji na kufikishiwa huduma hiyo.

Pia, amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme kuongeza kasi ya kusimika nguzo na kujenga miundombinu katika maeneo yaliyosalia ili wananchi wengi zaidi waweze kufikiwa na kuunganishiwa huduma ya umeme.

Amesisitiza kuwa shule, zahanati na maeneo mengine muhimu ya kutolea huduma za kijamii yanapaswa kupewa kipaumbele katika kufikishiwa umeme ili kuongeza ufanisi na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Aidha Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata nishati ya uhakika.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo unalenga kuwezesha wananchi kutumia umeme katika shughuli za uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, kukuza biashara, kuongeza fursa za ajira na kuboresha huduma za kijamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita ameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote vya Mkoa wa Shinyanga, akieleza kuwa hatua hiyo imefungua fursa mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.

Amesema upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini umeendelea kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za uzalishaji na ajira pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Herini Mhina, amesema Wakala unaendelea kutekeleza miradi ya kufikisha huduma ya umeme katika vitongoji mbalimbali nchini ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi, hususan katika maeneo ya vijijini, wanapata huduma hiyo.

Mhina amesema REA itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kupanua wigo wa upatikanaji wa umeme na kuwawezesha wananchi kutumia nishati hiyo katika shughuli za kiuchumi, uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii.

Nao wananchi wa Kitongoji cha Mwanubi wameishukuru Serikali kwa kuwafikishia huduma ya umeme katika kitongoji chao, wakieleza kuwa hatua hiyo itachochea shughuli za kiuchumi na kijamii na kuboresha maisha yao.

Wamesema ujio wa umeme utafungua fursa mpya za biashara na uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu katika eneo hilo.

Hafla ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Mwanubi ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia REA za kupanua wigo wa upatikanaji wa umeme vitongojini na kuhakikisha nishati hiyo inakuwa kichocheo cha maendeleo endelevu ya wananchi.

Related articles

Recent articles