26.3 C
New York

Idi Amin; Utata wa ‘birthday’, usaliti na udikteta wake (9)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

“KAMA hamtaki kupigana, nitapigana peke yangu.” Ni kauli aliyoitoa Idi Amin kuwaambia wanajeshi wake waliomfuta Machi, 1997, wakimuomba ajiuzulu baada ya kuzidiwa na Tanzania katika uwanja wa vita. Endelea …

Kauli hiyo ilifuatiwa na hatua ya Idi Amin kumfuta kazi aliyekuwa kiongozi mwandamizi wa jeshi, Yusuf Gowon. Aprili, 1997, Idi Amin alilazimika kutoroka kwa helikopta baada ya wanajeshi wa Tanzania kuuteka Mji Mkuu wa Kampala.

Idi Amin alikimbilia Mashariki mwa Uganda, kabla ya kutoroka moja kwa moja na kukimbilia Libya, ambako aliweza kuishi hadi mwaka 1980, kabla ya kuhamishia makazi Saudi Arabia.

Akiwa huko, taarifa zinaeleza kuwa familia ya kifalme inayoongoza nchi hiyo ilimpa kiasi kikubwa cha fedha ikimtaka kuachana na siasa. Pia, aliishi kifalme katika Hoteli ya kifahari ya Novotel mjini Jeddah.

Brian Barron, mwandishi wa habari wa BBC aliyeripoti Vita ya Uganda–Tanzania, pamoja na mpigapicha wake, Mohamed Amin, walibahatika kufanya mahojiano na Idi Amin akiwa Saudia.

Katika mahojiano hayo, Idi Amin alisisitiza kuwa bado Uganda inamuhitaji lakini hakuwa tayari kuzungumzia udikteta na ukatili aliofanya wakati wa utawala wake.

Januari, 1989, Idi Amin aliondoka uhamishoni bila kuwataarifu wenyeji wake (Serikali ya Saudi Arabia). Akiwa na mmoja ya watoto wake wa kiume, walifunga safari hadi Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC) na kuiacha familia mjini Jeddah.

Mpango wa kwenda Zaire ulikuwa na lengo moja tu; kuunda kikundi cha waasi ili kuiteka Uganda, ambayo wakati huo ilikuwa kwenye machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hata hivyo, licha ya kughushi hati za kusafiria ya Zaire, Idi Amin aligundulika akiwa Uwanja wa Ndege wa N’djili na ndipo alipokamatwa na vyombo vya dola. Serikali ya Zaire ilikasirishwa na ujio wake na ikaanza mchakato wa kumuondoa.

Saudi Arabia iligoma kumpokea kwa madai kuwa alivunja uaminifu alipoondoka bila kuaga, licha ya kwamba alipokelewa awali na kupewa hifadhi.

Serikali ya Zaire iliamua kumpeleka Senegal kwa makubaliano kuwa nchi hiyo ingempeleka Saudi Arabia. Hata hivyo, Taifa hilo la Kiarabu liliendelea kukataa kumpokea. Senegal iliamua kumrejesha Zaire.

Baadaye, Mfalme wa Morocco, Hassan II, aliingilia kati na Serikali ya Saudi Arabia ikakubali kumpokea. Aliporejea, aliahidi mambo matatu; hatojihusisha tena na siasa, jeshi, na kuzungumza na waandishi wa habari.

Julai 19, 2003, mmoja ya wake zake wanne, Nalongo Madina, aliibuka na taarifa kuwa Idi Amin yuko mahututi katika Hospitali ya King Faisal mjini Jeddah, akisumbuliwa na ugonjwa wa figo.

Bi. Madina alimtaka Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kumruhusu Idi Amin arudi ili kumalizia siku za mwisho wa uhai wake akiwa nchini kwake. Jibu la Rais Museveni lilikuwa rahisi tu, kwamba Idi Amin angelipia dhambi zote alizofanya endapo angerejea Uganda.

Related articles

Recent articles