Na Hassan Mwasha, Gazetini
KWA miaka mitatu mfululizo tangu aliposajiliwa mwaka 2023, amekuwa kwenye kiwango kile kile kutoka mechi moja hadi nyingine. Na inapotokea siku mbaya kazini, basi timu hukosa ubora fulani hivi ndani ya uwanja.
Unaweza usimkute sana kwenye takwimu za vinara wa ufungaji mabao. Unaweza usikutane naye pia unapotaka wanaoongoza kwa pasi za mabao (asisti), lakini haiondoshi umuhimu wake kikosini.
Nafasi yake kama injini ya timu ipo kwenye uwezo wake wa kutekeleza kwa ufanisi na kwa kiwango kile kile majukumu yote makubwa ndani ya uwanja.
Kwanza, atakupa huduma kama kiungo. Atacheza katika kila nafasi isiyo na mtu pembeni na katikati ya uwanja. ‘Mapafu ya mbwa’ aliyonayo yanampa uwezo wa kufanya hivyo.
Sekunde chache za mchezo utamkuta kulia, wakati mwingine atakwenda kushoto, na dakika kadhaa baadaye utamuona akiratibu mashambulizi akiwa katikati ya uwanja.
Wakati mwingine, atasogea na kuwa nje ya boksi au kuingia kabisa. Inaweza isiwe rahisi kujua namba yake maalumu anayocheza. Ni winga ya kulia, kushoto, kiungo wa kati au kiungo mshambuliaji?
Kwa lugha rahisi, mara zote Maxi Nzengeli hubeba majukumu ya ‘spea’ inayotumika wakati wowote kwenye eneo la kiungo au ushambuliaji.
Ubunifu, uwepo wa kupiga na kasi yake vimekuwa changamoto kubwa kwa walinzi wa timu pinzani na Yanga imenufaika vya kutosha kupitia faulo anazochezewa.
Usumbufu wake umekuwa ukiziharibia shepu safu za ulinzi, hivyo wachezaji wengine wa Yanga kupata nafasi ya kupenya na kujitafutia nafasi ndani ya boksi.
Pili, kwa kiwango na ufanisi ule ule, amekuwa na mchango mkubwa katika majukumu ya ulinzi na hii ni moja ya faida kubwa wanazopata Yanga.
Kwamba mbali ya kuwa na mabeki wanne, naye amekuwa akiwaongezea idadi kutokana na uwezo wake wa kurudi kuisadia timu inapokuwa kwenye presha ya kushambuliwa.
Ni mara nyingi tu utamkuta ‘akikata umeme’ katika mashambulizi ya timu pinzani, aidha akianzia kwenye kiungo wa ulinzi au nyuma kabisa.
Kubwa zaidi ni uwezo wa kulinda uwezo na ubora wake kwa misimu mitatu mfululizo aliyocheza Yanga na Tanzania kwa ujumla. Amebaki kuwa ni yule yule tangu mwaka 2023.
Kwa sifa hizo, kwanini Maxi Nzengeli asiwe ndiye ‘x-factor’ wa Yanga? Nimefunga mjadala na kukaribisha mitazamo, ikiwamo inayoweza kukinzana na hoja yangu hii.


